Serikali imetoa wito kwa Wataalam wa Maabara za binadamu nchini, kuionea wivu taaluma yao kwa kuwa ina mchango katika utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mkuu wa Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko hii leo Oktoba 2, 2024 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la 37 la Kisayansi la Wataalamu wa Maabara za Afya nchini na Kongamano la 23 la Kisayansi la HUOQAS na Mkutano Mkuu wa Mwaka.

Amesema, “wito wangu kwenu ioneeni wivu, muipende na kuithamini taaluma yenu, msikae pembeni mnapoona kuna changamoto semeni bila kuogopa. Wataalamu wa Maabara bila ninyi tiba haiwezi kufanyika na mfanye kila mtu awaheshimu.”

Aidha, Dkt. Biteko ameelekeza waajiri nchini kuruhusu watumishi wao wa kada ya maabara kushiriki katika makongamano ya kitaaluma huku akiwataka washiriki kujifunza kupitia mada zitakazowasilishwa na baadaye kuwashirikisha wataalam wenzao ambao hawakuhudhuria.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itafanyia kazi changamoto zote zilizowasiliahwa na MeLSET na kuitaka Wizara kuchukua hotuba ya MeLSAT na kuzifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa, ili mwaka ujao kuwe na masuala mengine ya kuzungumza.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye sekta ya afya na hiyo inaonesha hatua kubwa imepigwa huku akitaja shilingi trilioni 1.2 zilizotumika kuboresha maabara za afya nchini, huku akitaja eneo lingine lililoboreshwa katika sekta hiyo kuwa ni vitendea kazi vya kiuchunguzi kwa uwepo wa vifaa vya kisasa zikiwemo mashine 13 za MRI Digital xray 346, ulta sound 476 na ufundishaji wa ubingwa bobezi.

Amesema, “maboresho hayo yamegusa pia Mfuko wa ufadhili wa Rais Samia ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu pekee umeshagharamia kiasi shilingi bilioni 9 ili kusomesha wataalamu wa sekta ya afya hapa nchini. Tumetanua wigo wa utalii wa afya kupitia uwekezaji huu uliofanywa na Mhe. Rais Samia.”

Naye Kaimu Mganda Mkuu wa Serikali, Dkt. Saitore Laizer amesema kuwa Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele kukuza vyama mbalimbali vya kitaaluma ili viweze kusaidia kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha sekta ya afya nchini.

Amesema, baada ya Serikali kuwekeza katika vifaa tiba na miundombinu pamoja na watumishi suala kubwa ni kuhakikisha kuna ubora wa huduma za afya na kuwa hicho ni kipaumbele ili mambo yote yaliyofanyika yaweze kuwa na tija.

Awali, Rais wa Chama Cha Wataalam wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT), Yahya Mnung’a alisema lengo la Kongamano hilo ni kuwakutanisha wataalam na kutatua changamoto za kitaaluma katika maabara za binaadamu pamoja na uwepo wa maonesho ya vifaa vinavyotumika katika maabara za binadamu.

“Maabara ya Afya ya Jamii ya Tanzania imekuwa ikifanya kazi nzuri na maabara yetu ni kati ya Maabara tatu bora barani Afrika. Tunaiomba Serikali iridhie ombi letu la kupandisha hadhi maabara hii ili kuwa Taasisi kwa kuwa inafanyakazi kubwa ndani na nje ya nchi,” amesema Mnung’a.

Akiongea katika Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wataalamu wa Maabara za Afya Afrika (FeLPA), Mulate Mubanga amesema kuwa idadi kubwa ya watu hupata madhara kwa kutumia dawa bila kufanya vipomo vya maabara na kuwa ni vyema Serikali barani Afrika pamoja na wadau wa sekta hiyo kupatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 3, 2024
Kongamano Jotoardhi kuyakutanisha Mataifa 13 Nchini