Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi na usimamizi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) km 112.3, sehemu ya Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala (km 60) kwa kiwango cha lami na kumtaka Mkandarasi Kampuni ya AVIC kuwasilisha mpango kazi utakaomuwezesha kukamilisha ujenzi ifikapo mwezi Machi, 2025.
Bashungwa ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akikagua ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ambapo amemsisitiza Mkandarasi huyo kuongeza nguvu kazi, mitambo na kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati kama ilivyopangwa kwenye mkataba.
“Naibu Katibu Mkuu, hakikisha unakaa na Mkandarasi AVIC ili tuone mpango kazi wake ambao utaonesha ujenzi wa barabara hiyo kukamilika mwezi wa tatu mwakani kama mkataba unavyotaka”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemuagiza Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) anayejenga sehemu ya kwanza ya barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma kutoka Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Dry Port (km 52.3) kuhakikisha anakamilisha sehemu hiyo kufikia mwezi Desemba, 2024 kwa kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza katika mradi huo.
Amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde kusimamia kwa karibu ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma kwa kufanya ukaguzi na kutumia mikataba kuwabana Makandarasi wababaishaji na wazembe wasipewe fursa ya kupewa kazi nyingine.
Kadhalika, Bashungwa ameeleza Mikakati ya Serikali ya kupunguza msongamano na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika mji wa Dodoma kwa kupanua sehemu za barabara kuu zinazoingia ndani ya jiji hilo kuwa njia nne ambazo ni barabara ya Dodoma mjini – Ikulu Chamwino, Dodoma Mjini – Msalato na Dodoma Mjini – Mkonze (SGR).
Awali, akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Msimamizi wa Mradi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Herman Laswai amesema kuwa tayari Wakala umeshamuelekeza mkandarasi AVIC kutatua changamoto ya vifaa aliyonayo na tayari walishamuandikia barua ya onyo ya kutokumuongeza muda.
Kwa upande wake, Mhandisi kutoka kampuni ya Inter – Consult, Injinia. Deogratius Nyambo ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma sehemu ya Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Dry Port (km 52.3) kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 83.6 na umeweza kutoa fursa za ajira kwa wazawa 505.
Naye, Mhandisi kutoka Kampuni ya PACE, Injinia Daniel Nila ameeleza ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma sehemu ya Ihumwa – Matumbulu – Nala (km 60) umefika asilimia 79.1.