Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wito kwa wadau wote kuungana kuhakikisha kila mlipa kodi analipia kodi inayostahili, ili kukuza uchumi wa nchi hususani Mkoa wa Dar es salaam.
Chalamila ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Kodi lililofanyika ukumbi wa Julius Nyerere(JNICC) na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka TRA na OASIS FINANCIAL SERVICES.
Chalamila ameipongeza taasisi ya OASIS kwa kuwa daraja Kati ya TRA na wafanyabiashara katika kutoa elimu ya kikodi ili kupunguza migogoro ya kikodi isiyo ya lazima
Aidha, amesema kuwepo kwa mtindo wa “Control Number” imesaidia sana hivyo amependekeza wataalamu kuleta teknolojia nyingine iliyo pana zaidi itakayoweza kusaidia katika upande wa ulipaji Kodi.
Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Oasis Group, Stambuli Myovela, alieleza kuwa kongamano hilo limelenga kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya kodi.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni ili kupata suluhisho endelevu na kwamba OASIS imejitolea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato.