Maseneta wa Bunge la Seneti Nchini Kenya, wameendelea kujitenga na muswada uliowasilishwa na Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei, unaolenga kuongeza muda wa Rais na Wabunge kuhudumu kutoka miaka mitano hadi saba.
Seneta wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kamau ambaye pia ni mwanachama wa chama cha UDA, amesema kwasasaTaifa linafaa kuangazia maswala muhimu kwa Mwananchi wa kawaida na sio Viongozi kujiongezea muda wa kuhudumu, kauli ambayo iliungwa mkono na Seneta wa Bungoma, David Wakoli.
Mapema wiki hii, Seneta wa Nandi Samson Cherargei, alipeleka Muswada kwa bunge la Seneti, akitaka kufanyiwa marekebisho kifungu cha 136 cha katiba ya Kenya ili kuongeza muda wa kuhudumu kwa viongozi waliochaguliwa.
Alisema, anashauri muda huo uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba, kwani kipindi cha sasa cha miaka mitano hakitoshi kwa Viongozi waliochaguliwa kutimiza ahadi zao.