Baadhi ya Watu wameendelea kutoa lawama kwa Vyombo vya usalama na wasimamizi wa safari, kufuatia vifo vya watu 78 vilivyotokea baada ya boti iliyokuwa imejaza watu kupita kiasi kupinduka kwenye Ziwa Kivu, lililopo mashariki mwa Kongo
Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini, Jean-Jacques Purusi alisema idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka na kwamba taarifa ambazo alipatiwa na mamlaka ya eneo hilo zilieleza kwamba Boti hiyo ilikuwa imebeba Watu zaidi ya 277.
Purusi ambaye alikuwa akiongea kwa simu, amesema chombo hicho cha Usafiri kiliondoka Bandari ya Minova, katika jimbo la Kivu Kusini mchana wa Oktoba 3, 2024 ikielekea Goma, katika jimbo la Kivu Kaskazini na wasimamizi wanalaumiwa kwa kujaza watu bila kuangalia hatari inayoweza kujitokeza.
Boti hiyo, ilizama wakati ikijaribu kutia nanga umbali mfupi kutoka Bandari ya Kituku, huku mashuhuda wakisema baada ya kuzama waokoaji waliopoa miili 50 na kudai kuwa ajali hiyuo ni mbaya na imetokana na kutofuatwa kwa sheria za usafirishaji wa Bahari.
Hata hivyo, Mamlaka ya Kongo mara nyingi zimekuwa zikimeonya juu ya upakiaji kupita kiasi na kuapa kuwaadhibu wale wanaokiuka hatua za usalama za usafirishaji wa majini, lakini katika maeneo ya mbali ambako abiria wengi wanatoka, wengi hawana uwezo wa kumudu usafiri wa umma kwa barabara chache zilizopo.
Juni, 2024 Boti iliyokuwa imejaza mizigo mingi ilizama karibu na Mji mkuu wa DRC, Kinshasa na abiria 80 walipoteza maisha ajali iliyotokea mara baada ya ile ya Januari 2024 baada ya watu 22 kupoteza maisha Ziwa Maî-Ndombe na Aprili 2023, sita walifariki na 64 kupotea huko Ziwa Kivu.