Boniface Gideon – Tanga.

Jeshi la Polisi Mkoani Tanga linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu wa familia moja, yaliyotokea Septemba 23, 2024 katika eneo la ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Korogwe, Kijiji na Kata ya Sindeni Wilayani Handeni.

Akizungumza Wandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi Almachius Mchunguzi, alisema katika tukio hilo miili ya watu watatu iligundulika ndani ya gari aina ya Toyota IST yenye namba T 305 EAL.

Amesema, kati ya miili hiyo ya watu watatu iligundulika pia mwili wa aliyekuwa Mkaguzi wa Ndani (Internal Oditor wa Halmashauri ya Korogwe, Jonais Edward Shayo (46) na mtoto wake Dedani Lameck Shayo (8) na Salha Bakari Hassani (Dada wa Kazi) (18) Mkazi wa Bagamoyo.

“Jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi na msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita ambao ni Benard Adam Kizughuto (31) mkulima na mkazi wa Msambiazi Wilaya ya Korogwe, Marko John Jambia Rajabu Mhilu(28) mkulima mkazi wa Lushoto na Peter John Jambia Johson (31) mkulima mkazi wa Msambiazi Korogwe.

Wengine ni Hassani Ramadhani Bakari Kitombo Jombi (53) mkulima na mkazi wa Kwamaraha Wilaya ya Handeni, James Mkama Teacher (42) Mfanyabiashara na mkazi wa Mtonga Wilaya ya Korogwe na Omari Saleh Mwiba (20) mkulima na mkazi wa Kwamaraha Wilayani Handeni.

Kamanda Mchunguzi alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea kukamilishwa, ili hatua nyingine za kisheria zifuatwe.

Hata hivyo, alisema Jeshi hilo linalaani vikali vitendo vyote vya kihalifu na halitomuonea muhali wala halitasita kuwachukulia hatua za kisheria mtu yeyote au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitend vya kihalifu.

Dkt. Magembe: Shughulikieni changamoto kwenye maeneo yenu
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 4, 2024