Angela Msimbira, OR-TAMISEMI.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Miundombinu), Mhandisi Rogatus Mativila amewaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha wanahamasisha uanzishwaji wa vituo vya kulelea Watoto Wadogo Mchana vya Kijamii katika vijiji/mtaa na kuwasilisha taarifa hii ifikapo Januari 30, 2025.

Mhandisi Mativila ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma alipomuakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Ndunguru wakati akifungua mafunzo ya Kitaifa ya Uratibu na Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto kwa Maafisa ustawi wa Jamii wa Mikoa na Halmashauri.

Amesema, katika kipindi hiki ukuaji na ujifunzaji wa watoto unakwenda kwa haraka sana huku mazingira yanayowazunguka yakiwa na mchango mkubwa wa kuamua hatima ya maisha yao, kivyo uwekezaji wa mapema katika huduma bora na kwa wakati kunawezesha kukuza rasilimali watu yenye tija kwa familia, jamii na taifa.

Amesema pia wahakikishe wanasimamia kwa ukamilifu Programu hii katika maeneo yao na taarifa za utekelezaji wa kila kipengele cha programu hii kuwezesha serikali kupata mafanikio na changamoto za Malezi na Makuzi ya watoto wa taifa hili.

Mhandisi Mativila amewataka kuendelea kutoa elimu kwa jamii kwa njia mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwenye malezi bora ya watoto.

Aidha, amewataka kuhakikisha wanawatambua na kuendelea kushirikiana na wadau wote wa MMMAM waliopo kwenye mikoa na halmashauri ili kuchangia utekelezaji wa programu hiyo.

“Pia hakikisheni vikao vya mapitio ya Programu vinavyowaleta wadau kwenye ngazi ya mkoa na halmashauri vinafanyika kama vilivyoelekezwa na Programu hii,” amesisitiza.

“Napenda kutoa rai kwenu mkawe mabalozi wazuri wa kuhakikisha watoto wadogo wenye umri wa miaka 0-8 wanapatiwa huduma zote za Malezi Jumuishi ikiwemo, Afya bora, Malezi yenye Mwitikio, Lishe toshelevu, Ujifunzaji wa Awali, na Ulinzi na Usalama.”

Serikali yawapa uhakika Wanawake juu ya uzazi salama
Serikali: Tunathamini mchango wa Viongozi wa Dini