Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kuishughulikia Sheria ya vyombo vya barabarani na kuharakisha mchakato wa kuwapatia Wazee vitambulisho maalumu vitakavyowasaidia kulipa nusu nauli kama ilivyo kwa wanafunzi na watu wenye ulemavu.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Wazee, duniani katika ukumbi wa ZSSF, Tibirinzi Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba na kuziagiza taasisi zote za Serikali, zinazotoa huduma za usatawi kwa Wazee, kuzishughulika haraka na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili Wazee hao.
Taasisi zilizopewa maagizo hayo ni Wizara ya Afya ambayo inatakiwa kuandaa madirisha maalumu Hospitali zote kutoa huduma bora za Wazee kwa kuwapa kipaumbele, pamoja na kuongeza madaktari bingwa wa magonjwa ya wazee na Wizara ya Fedha ambayo inatakiwa kuandaa bajeti maalumu ya kuendesha mabaraza ya Wazee pamoja na kufungua madirisha maalumu kwenye benki na vituo vyote vinavyotoa huduma za Fedha kuwapa kipaumbele Wazee hao.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali imeandaa na inaendelea kutekeleza Sera ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2014 ambayo imeweka mikakati madhubuti ya kusimamia maendeleo ya Wazee.