Naibu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amesema hatojiuzulu nafasi hiyo licha ya kuwasilishwa hoja bungeni ya kumuondoa madarakani.
Akilihutubia Taifa kutoka makazi yake rasmi ya Karen mjini Nairobi, Gachagua ameeleza kuwa atafika bungeni hii leo Oktoba 8, 2024 ili kujitetea.
Gachagua, amekuwa kwenye shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa na hata wananchi wanaomtaka ajiuzulu kutokana na tuhuma zinazomkabili za kujilimbikizia mali kinyume cha sheria, kuihujumu serikali na kutoa matamshi ya kuchochea ukabila.
Ameeleza kuwa baadhi ya mali zake alizirithi kutoka kwa nduguye marehemu Gavana wa zamani wa Kaunti ya Nyeri Nderitu Gachagua na aliitisha mkutano huo na waandishi wa habari ili kutoa utetezi wake kabla ya kuwasili bungeni baadaye leo.