Kuna Hadithi moja niliwahi kuisikia kuwa Kijana mmoja alimuona Mwalimu wake aliyewahi kumfundisha Shule ya Msingi, kwenye Sherehe ya Harusi ambayo yeye alikuwa ni mwalikwa hivyo akapata shauku ya kwenda kumsabahi, maana ni kitambo kilipita bila kuonana.

Kwa heshima Kijana alienda kumsabahi Mwalimu wake huyo akiwa na bashasha, akamuambia “je, unaweza kunitambua Mwalimu?’…..

Mwalimu alimjibu….. ‘Sidhani! naomba unikumbushe.”

Bila ajizi Mwanafunzi huyo akaanza kumsimulia Mwalimu akisema, “nilikuwa Mwanafunzi wako ulinifundisha Darasa la 3, na kuna siku niliiba saa ya Mwanafunzi mwenzangu kwasababu ilikuwa ya kipekee na ya kuvutia.”

Ukumbusho uliendelea, “yule Mwanafunzi mwenzangu alikuja kwako akilia kwamba saa yake imeibwa na ndipo wewe Mwalimu ukaamuru Wanafunzi wote Darasani tusimame kwenye mstari ulionyooka, tukitazama ukuta huku mikono yetu ikiwa juu na macho yetu tuyafumbe, ili uangalie mifuko yetu,” alisema Mwanafunzi huyo.

Aliendelea kusimulia kwamba, “nilianza kupata wasiwasi na hofu ya matokeo ya utafutaji ule nikiwaza aibu ambayo ningeipata baada ya Wanafunzi kugundua kuwa niliiba saa, maoni mbayo Walimu wangu wangeyapata kunihusu, kuitwa mwizi, kufukuzwa Shule na jinsi Wazazi wangu watakavyonichukulia.”

Anasema, “wakati nikiwaza yote hayo ghafla ikafika zamu yangu ya kuchunguzwa. Nilihisi mkono wako ukiingia mfukoni mwangu, ukatoa Saa na kuweka kikaratasi mfukoni mwangu nikashikwa na hofu, nikitarajia mabaya zaidi yangetangazwa. Nilishangaa hukufanya lolote na uliendelea kupekua mifuko ya wanafunzi wengine hadi ukafika mtu wa mwisho.”

“Upekuzi ulipoisha, ulituomba tufumbue macho na tukae kwenye viti vyetu. Niliogopa kukaa maana nilifikiri utaniita mara baada ya kila mtu kuketi huku nikiwa na shauku ya kujua kikaratasi kile kilikuwa na ujumbe gani na kwa haraka nikakifungua kwa kificho, kisha nikakisoma ….. uliandika, “ACHA KUIBA, MUNGU HAPENDI NA NI CHUKIZO KWA WATU, UTAAIBIKA,” alisema.

“Mapigo ya Moyo yalinienda kasi nikibashiri kinachokuja kutokea mbeleni na kilichofuata, baadaye uliionesha saa ukiwa mbele ya Darasa na ukampa mmiliki wake na hukutaja jina la aliyeiba wala hukuniambia neno lolote na hata hukuwahi pia kusimulia tukio hilo kwa mtu yeyote,” alizidi kusimulia.

Mwanafunzi anasema, “Katika kipindi chote nilichokuwa shuleni, hakuna Mwalimu au Mwanafunzi aliyejua kilichotokea. Tukio hili kwa kawaida lilinifundisha somo kubwa na niliamua moyoni mwangu kamwe kutojihusisha katika kuchukua chochote ambacho si changu.”

“Uliniepusha na aibu, uliniokoa na aibu pia uliilinda heshima yangu Mwalimu wangu, Je? sasa umenikumbuka, unakumbuka hadithi hii sasa Mwalimu? bila shaka huwezi kusahau kisa hiki kirahisi Mwalimu wangu, nini mimi,” alimwambia Mwalimu wake Kijana huyo,” aliisitiza.

Alipomaliza Mwalimu akajibu huku akitabasamu, “ninakumbuka vizuri tukio hili kwamba ni kweli niliikuta Saa mfukoni mwa Mwanafunzi lakini sikujua Saa hiyo iliyoibwa ilipatikana mfukoni mwa Mwanafunzi yupi siku hiyo, kwa sababu nilipekua mifuko yako na ya wote huku pia nikiwa nimefumba macho kama ninyi ila leo rasmi nimetambua ni nani aliiba ile Saa unaponiambia hivi sasa.” hili jibu lilimshangaza kijana yule na wote wakabaki wameduwaa.

Sikia nikuambie, kiukweli katika maisha, tunahitaji hekima kwa kila jambo tunalofanya kama Wazazi, Walimu, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Serikali n.k, tunapaswa kuwa na uwezo wa kufumba macho yetu kwa baadhi ya mambo kwani sio tabia zote mbaya zinahitaji adhabu zingine zinapaswa kuwa kama somo la maisha.

Wengine watahitaji kutiwa moyo, wengine kushauriwa na wengine kuwafuatilia, kwahiyo wewe Mwalimu au Kiongozi ama Mzazi, uwe mwenye kutia moyo siku zote na sio mtu wa kuvunja moyo, maana hatua unazochukua dhidi ya waliokukosea kama hadithi hii isemavyo, inaweza kubadilisha maisha na tabia za wakosaji.

Kagera: Wafanyabiashara acheni kukwepa Kodi - TRA
Malimwengu: Waoga Pombe kuponya majeraha