Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Matengenezo ya Barabara wa Siera Leone, Mohamed Kallon ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa madaraja na barabara kwa kutumia mawe.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kallon amesema wamefurahishwa na teknolojia hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inapunguza gharama za ujenzi pia kutumia malighafi zilizopo eneo husika.
Amesema, ujio wao hapa nchini ni kujifunza ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya katika maeneo ya mipango,ushirikishwaji wa wananchi na utumiaji wa teknolojia mbadala na kwamba kati ya agenda tano za Rais wa nchi yao ni kuilisha Siera Leone hivyo kitu muhimu ni kufungua barabara ili kuuza na kusafirisha mazao toka kwa wakulima.
“Wananchi wa Siera Leone ni wazalishaji na wengi wanaishi vijijini hivyo kwa kutumia teknolojia ya mawe itawarahisishia kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda kwenye masoko,” amesema Kallon
Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amesema kwamba matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara kama mawe yaliyopo kwenye eneo la kazi inapunguza gharama za ujenzi wa madaraja na barabara kwa zaidi ya asilimia 40.
Kuhusu ushirikwishaji wa vikundi vya kijamii kwenye ujenzi na matengezo ya barabara, Mhandisi Seff amesema kupitia mradi wa uboreshaji wa barabara za vijijini ambao ni mkopo rahisi toka Benki ya dunia ambao wanasaidia kuanzisha, kufundisha na kuviwezesha vikundi hivyo kufanya kazi za matengenezo ya barabara kwa weledi na umakini.
Amesema, “faida kubwa ya kuvitumia vikundi hivyo inapunguza gharama kwani vinatoka maeneo yale yale zinapopita barabara pia inasaidia kulinda miundombinu ya barabara ikiwemo alama za barabarani kwani wanatambua barabara ni mali yao.”
Hata hivyo, Mhandisi Seff aliongeza kusema kuwa wao kama TARURA wapo tayari kushirikiana na Siera Leone kwa kuwapatia wataalam wa kufundisha pale panapohitajika.