Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeanza ukaguzi katika eneo la viwanda lililopo Mbagala jijini Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyemtaka Mkurugenzi Mkuu wa NEMC kufika katika eneo hilo kutatua kero ya Maji yanayotiririka kutoka Viwandani kwenda katika makazi ya watu.

Akizungumza katika ziara hiyo mara baada ya ukaguzi uliofanyika katika kiwanda cha Camel Cement, Mkurugenzi Mkuu NEMC, Dkt. Immaculate Semesi amesema Waziri Mkuu alitaka kuhakikisha kwamba kero inayowapata Wananchi inatatuliwa kwa haraka.

Amesema, “Tunatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoyatoa juzi wilayani Temeke, tumefika na kukagua baadhi ya viwanda na tumejionea changamoto na athari za mazingira zinazotokana na kiwanda hiki.”

Dkt. Sware amewataka wenye viwanda kote nchini ambao hawajafanya tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) au wenye vyeti vya mazingira lakini hawafati matakwa ya vyeti hivyo, kuchukuliwa hatua za kisheria hadi kufikia Oktoba 30, 2024.

“Tunatoa wito na onyo kwa viwanda vya uzalishaji wa aina yoyote nchini lazima tufanye tathmini ya athari kwa mazingira na vile viwanda vyenye vyeti wazingatie matakwa ya vyeti hivyo vya mazingira, kama viwanda havifanya inavyotakiwa hadi kufikia oktoba 30,2024 kiwanda chochote nchini hakitafanya hivyo tutachukua hatua za kisheria.” aliisitiza Dkt. Sware.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Abdallah Chaurembo amemshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu kwa wakati na kuwataka wenye viwanda kushirikiana na Wananchi, ili kumaliza tatizo hilo linalowakabili wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Kiwanda Cha Camel Cement Afisa Usalama, Afya na Mazingira kiwanda hicho, Amir Dilawa amesema amepokea maelekezo ya NEMC na kuahidi kurekebisha mapungufu yote yaliyobainika.

Oktoba 5, 2024, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Temeke alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa NEMC kutembelea viwanda vya Mbagala vinavyotiririsha maji kwenye makazi ya watu agizo ambalo Mkurugenzi Mkuu wa NEMC amelitekeleza.

Wafanyakazi wa OYA mbaroni kwa mauaji wakidai rejesho
Wananchi tusiwachague Viongozi ambao si Watanzania - RC Mwasa