Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amewasili nchini Finland kwa ziara ya kikazi kuanzia Oktoba 8 – 11, 2024.
Alipowasili kwenye Uwanja wa ndege jijini Helsink, Waziri Kombo alipokewa na Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting na Balozi wa Tanzania nchini Finland mwenye makazi yake Stockholm, Sweden, Grace Ulotu.
Katika ziara yake hiyo, Waziri Kombo pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Elina Valtonen Oktoba 9, 2024.
Aidha, Kombo na Mwenyeji wake watashiriki kikao cha pili cha mashauriano ya kisiasa (political consultations) kama wenyeviti wenza wa mashauriano hayo. Kikao hicho kitajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili.
Vile vile, Kombo na ujumbe wake watashiriki mikutano ya kibiashara inayolenga kuvutia kampuni kubwa za nchini Finland kuja kuwekeza Tanzania katika maeneo mbalimbali kama vile misitu, nishati, TEHAMA, utalii na elimu.
Katika ziara hiyo, Waziri Kombo ameambatana na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE).