Fredy Kibano – Tabora.

Mkurugenzi Msaidizi, Elimu ya Watu Wazima, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwalimu Ernest Hinju amewataka Maafisa Elimu Watu Wazima wa Mikoa na Halmashauri nchini kufanya kazi kwa ufanisi na weledi, ili kuleta mageuzi kwenye Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.

Mwalimu Hinju ametoa wito huo wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa Elimu Watu Wazima chenye lengo la kutathmini utendaji kazi wao, kilichofanyika Manispaa ya Tabora katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Mwalimu Ernest Hinju amewataka Watendaji hao kutumia fursa ya kikao kazi hicho kufanya tathmini ya utendaji kazi wao nchini, ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.

Amesema, “kikao hiki kitumike kufanya tathmini ili kuona kwa kiasi gani tunatekeleza kwa ufanisi shughuli zote za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi na hatimaye mje na mikakati ya kuboresha utendaji kazi.”

Mwalimu Hinju amesema, kikao hicho pia kitapitia maazimio ya kikao kama hicho kilichofanyika mkoani Morogoro mwaka 2023 na kutoa fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu wa namna bora ya kutatua changamoto zinazoikabili Elimu ya Watu wazima ikiwa ni pamoja na kudumisha umoja, ushirikiano na upendo miongoni mwa Maafisa Elimu hao.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu wa Mkoa wa Tabora, Aron Vedasto ameishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuandaa kikao kazi hicho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya juma la Elimu ya Watu Wazima mkoani Tabora kwani wataweza kujitathmini kiutendaji kama mkoa.

Ameahidi kuwa, watahakikisha wanainua Elimu ya Watu Wazima kwani kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha mkoa huo ndio unaoongoza kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Madaktari Bingwa waiwezesha Sikonge kuanza upasuaji
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 9, 2024