Tanzania na Finland zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) kuhusu kufanya rasmi Mashauriano ya Kisiasa kati ya nchi hizo mbili.
Uwekaji saini huo ulifanyika Oktoba 9, 2024 jijini Helsinki na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo kwa niaba ya Tanzania na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Elina Valtonen kwa niaba ya Serikali ya Finland.
Makubaliano hayo yanatoa fursa kwa nchi hizo kuwa na kikao cha Mashauriano ya Kisiasa kwa kupokezana kila mwaka ili kujadili na kukubaliana maeneo ya kipaumbele ya kushirikiana yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Tukio hilo limehudhuriwa na maafisa wakuu wa pande zote mbili, akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Finland, ambaye makazi yake yako Stockholm Sweden, Grace Olotu na Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting.
Wengine ni Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika, Balozi Swahiba Mndeme na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, Dkt. Gift Kweka.