Afarah Suleiman, Babati Manyara.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bagara, Joel Mariki aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Septemba 14, 2024 katika Mlima Kwaraa Mjini Babati Mkoani Manyara, amepatikana katika Kijiji cha Galapo ambapo msamaria mwema alimfikisha Hospitali ya Mkoa wa Manyara akiwa na majeraha kwenye mwili wake huku akiwa amedhoofika.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Queen Sendiga aliyefika Hospitalini hapo kumjulia hali mtoto huyo kisha akazungumza na Wanahabari ambao hawakuweza kupata picha za mtoto huyo ambaye yupo kwenye uangalizi wa karibu na madaktari.


Baba mzazi wa kijana huyo,  Johanes Mariki ameelezea furaha yake baada ya kumpata kijana wake akiwa hai na kuwashukuru Watanzani wa dini zote ambao walimfanyia maombi mpaka kupatikana kwa mtoto huyo, ambaye anadaiwa alikwenda kufanya mafunzo ya vitendo na Wanafunzi wenzake, kisha kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Catherine Magali amekiri kumpokea mtoto huyo na kusema kuwa kwasasa anaendelea na matibabu.

Picha: Rais Samia aongoza kikao Baraza la Mawaziri
Maisha: Waleta dharau eti nao wanashangaa kudharauliwa