Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, linamshikilia Jaina Mchomvu kwa tukio la mauaji ya mtoto aitwaye Mariam Juma (12), mkazi wa Mrombo Arusha aliyekutwa ameuawa huku mwili wake ukiwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya shingoni na maeneo mbalimbali na mwili wake kufichwa kwenye uvungu wa kitanda nyumba ya jirani yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Justine Masejo amesema awali mtoto huyu alikuwa ametumwa dukani toka asubuhi lakini hakurejea na ilipofika mchana wazazi wake walianza kumtafuata maeneo mbalimbali baada ya kuingiwa na wasiwasi.

Amesema, “hadi sasa tunawashikilia watu watatu akiwepo Jaina Mchomvu Mama mwenye nyumba ambaye amekamatwa na askari Polisi huko Mabogini Moshi, Mkoani Kilimanjaro alikokimbilia kujificha baada ya tukio hili kubaainika, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha kwa ajili ya uchunguzi zaidi.”

Kamanda Masejo amesema baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa Jaina Mchomvu alihojiwa na kukiri kutenda tukio hilo la mauaji ya mtoto huyo na kwamba uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali, ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 13, 2024
Rais Samia alivyowasili Mwanza katika kilele mbio za Mwenge