Johansen Buberwa – Kagera.
Mkoa wa Kagera umevunja rekodi ya Kitaifa ya kwa nafasi ya kwanza katika usimamizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, iliyotembelewa na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024.
Wakizungumza katika Uwanja wa Ndege baada ya kumpokea Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa baadhi ya Wananchi akiwemo Rebecca Magoma na Joyce Lobozi wamesema mkoa huo unazidi kupiga hutua kubwa za kimaendeleo, ukilinganisha na miaka iliyopita.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa Hajat Mwasa aliwashukuru Wananchi wa Wilaya zote za Kagera na kusisitiza kuwa ushindi huo wa Kombe na Cheti si wa mtu mmoja, bali ni wa Wanakagera.
Amesema juhudi za kushinda zilifanikishwa na Wanakagera ambao walijitoa kwa hali na mali kwa kutumia maarifa na akili zao, pamoja na kukataa kurudi nafasi za nyuma zilizokuwa zimezoeleka kwa miaka ya mingi.
“Nawashukru sana kila mmoja kwa nafasi yake Wana Kagera nawapenda halafu nawapenda sana,” alisema Mwassa.
Ushindi huo, umekuja kutokana na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ambayo ilipitiwa na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru na ulitangazwa wakati wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 mkoani Mwanza.
Tukio hilo pia liliambatana na hitimisho la Wiki ya Vijana Kitaifa na Kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Oktoba 14, 2024.