Wabunge wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamesisitizwa kuyabeba majukumu waliyopewa kwa uzito unaostahili, huku wakiweka mbele maslahi ya umma wakati wanatekeleza majukumu yao.
Kauli hiyo, imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), alipokutana na Wabunge hao jijini Dodoma Oktoba 17, 2024.
Waziri Kombo amewasisitiza wabunge hao kutumia nafasi walizopewa katika Bunge hilo kuhimiza umoja, mshikamano na ushirikiano baina ya nchi wanachama wa umoja huo.
Amesema, “nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) tokea enzi zimekuwa na umoja wa kindugu, hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa umoja huo unaendelezwa, unaimarishwa na kuenziwa ili kutimiza lengo la Wakuu wa Nchi la kuwa na mtangamano imara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
Waziri amewaambia wabunge hao kuwa ili kutimiza majukumu yao ipasavyo katika chombo hicho muhimu katika jumuiya, wanatakiwa kujua mipango mbalimbali ya Serikali ili waweze kuisemea na kuitetea vyema.
Amewahimiza kuirejea mara kwa mara Ilani ya Chama cha Mapinduzi – CCM, ili kuelewa malengo yanayotakiwa kufikiwa katika mtangamanao wa Afrika Mashariki na mipango mingine ya maendeleo ya Serikali kama vile, Mpango wa Mwaka wa Bajeti ya Serikali.
Aidha Waziri Kombo ameeleza kuwa, Wizara yake ipo tayari kupokea ushauri wakati wowote kutoka kwa Wabunge hao unaolenga kuboresha utekelezaji mzuri wa programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
”Wizara ina Naibu Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo; Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi; Wakurugenzi wa Idara zinazotekeleza masuala ya Afrika Mashariki na nipo mimi mwenyewe, Waziri, njooni tushauriane wakati wowote yanapoibuka masuala yanayohitaji ushauri au mwongozo wetu,” alisisitiza Balozi Kombo.
Amehitimisha maelezo yake kwa Wabunge hao kwa kuwakumbusha kuwa Wizara yake ina dhamana kubwa ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayohimiza diplomasia ya uchumi, hivyo aliwataka kutumia nafasi walizonazo kutangaza fursa za Tanzania ikiwa ni pamoja na fursa ya Tanzania kupakana na nchi nyingi ambazo hazina bandari.
Kwa upande wa Wabunge, wakiwakilishwa na Katibu wao, Ngwaru Maghembe wamemshukuru Waziri kwa kutenga muda wa kukutana nao na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Wizara katika kufanikisha majukumu ya bunge kwa kuzingatia maslahi ya nchi na Jumuiya kwa ujumla.
Katika kikao hicho ambacho kilikuwa cha kujitambulisha, Waziri Kombo aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo.
Kwa upande wa Wabunge walioshiriki kikao hicho ni Dkt. Ngwaru Maghembe (CCM), Mashaka Ngole (CUF), Kachwamba Ansar (CCM), Nadra Juma Mohamed (CCM) na Mbunge Mteule, Gladness Salema (CCM).