Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amekutana na Uongozi wa Chama cha Wauguzi na Ukunga Tanzania – TANNA, kujadili mpango kazi wa utekelezaji wa hoja za wauguzi zilizo jitokeza wakati wa mkutano wa mwaka uliofanyika Mei 12, 2024 ili kuongeza ubora wa Huduma kwa wananchi.
Katika majadiliano hayo, Mhagama amesema anatambua mchango na kazi kubwa inayofanywa na wauguzi na wakunga katika sekta ya afya hivyo anawapongeza kwa kazi nzuri inayofanyika katika kuwahudumia wananchi.
Amesema, moja ya jukumu kubwa analofanyia kazi kwa sasa ni kuhakikisha wauguzi na wakunga wanapandishwa madaraja kama ilivyo kwa kada zingine na kwamba wakati wanafanyia kazi changamoto zao pia wasaidie kusimamia maadili kwa wauguzi, ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.
Mhagama ameongeza kuwa, Serikali kupitia wizara ya Afya inafanya kazi kuhakikisha inatatua changamoto wanazokabiliana nazo wauguzi na wakunga hivyo waendelee kuchapa kazi kwa kufata miiko na maadili ya taaluma wanapo wahudumia wananchi.
Kwa upande wake Rais wa TANNA, Alexender Baluhya amesema Wauguzi na Wakunga wanaimani kuwa Serikali itatatua changamoto zao kwa wakati, ili kuleta tija katika utendaji kazi ma kwamba lengo la kukutana na Waziri Mhagama ni kufuatilia utekelezaji wa hoja za Wauguzi zilizotolewa katika mkutano wa mwaka, uliofanyika Mkoani Tanga ikiwemo kupandishwa madaraja.