Kwa mara nyingine tena, Tanzania imeibuka Mshindi kwa kujinyakulia tuzo nne katika Tuzo za Utalii zinazotolewa na World Travel Awards ya Nchini Marekani.
Tuzo hizo ni pamoja na Eneo Bora la Utalii Afrika (Tanzania), Bodi Bora ya Utalii Afrika (TTB), Hifadhi Bora ya Afrika (Serengeti), na Kivutio Bora cha Utalii Afrika (Mlima Kilimanjaro).
Tuzo hizi zimetolewa katika hafla iliyofanyika usiku wa kuamkia leo October 19, 2024, Mjini Mombasa, Kenya, na kupokelewa na Viongozi wa Wizara ya Utalii, TTB, na TANAPA, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii Nkoba Mabula, Mjumbe wa Bodi ya TANAPA CPA Hadija Mohamed, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii, Ephraim Mafuru, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, Betrita Lyimo na Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Stephano Msumi.
Ushindi huu unaifanya Serengeti kuendelea kuwa Hifadhi Bora ya Afrika kwa miaka sita mfululizo (2019, 2020, 2021, 2022, 2023, na 2024), pia Bodi ya Utalii Tanzania imekuwa Bora Afrika kwa miaka mitatu mfululizo (2022, 2023, na 2024) ambapo Nkoba amesema ushindi umechagizwa na sera za Rais Dkt. Samia kuvutia Watalii na kukuza utalii kwa ujumla kupitia Royal Tour.
Tuzo za World Travel zilianzishwa mwaka 1993 kwa lengo la kutambua, kutunza, na kusherehekea ubora katika sekta zote muhimu, ikiwemo usafiri, utalii, na ukarimu, leo hii World Travel Awards inatambulika Kimataifa kama alama ya ubora katika tasnia mbalimbali.