Mwezi mmoja baada ya ziara ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini China, Tanzania imefanikiwa kusaini Hati ya Ushirikiano ya uwekezaji na mafunzo na Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Kielekroniki ya China (CECIS LTD) utakaowezesha kampuni zaidi ya 600 za vifaa vya Kompyuta kuwekeza nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla na Mwenyekiti wa Kampuni ya CECIS, Guo Zhaoping na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa hati hiyo, Mahundi amesema uwekezaji huo utaongeza ujuzi kwa vijana na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utengenezaji wa kompyuta na vifaa vingine vya Kielektroniki utakaowezesha kupiga hatua kubwa katika masuala ya uchumi wa kidijitali.
Amesema, “makubaliano haya ni matokeo ya ziara ya Rais Samia nchini China aliyoifanya hivi karibuni, Kampuni hii ni wabobezi wa masuala ya usalama wa mitandao hivyo elimu waliyonayo itawawezesha vijana kujifunza kwani tunahitaji wataalamu wengi zaidi wa TEHAMA nchini” amesema Mhandisi Mahundi.
Akitoa salamu katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Abdulla amesema uwekezaji huo utatoa fursa kwa watanzania kujifunza na kupata ajira huku akiihakikishia kampuni hiyo ulinzi na usalama unaotokana na uwepo wa sera na sheria nzuri kwa wawekezaji na kusema Tanzania ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), inayo fursa kubwa kwa wawekezaji kupata soko la zaidi ya watu milioni 600.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya huduma za mawasiliano ya kielekroniki ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia wa Kamati ya Kampuni hiyo, Guo Zhaoping amesema uwekezaji huo umefuata misingi ya nchi za Tanzania na China na kwamba unalenga kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
“Kampuni yetu inafanya uwekezaji katika mambo makuu matano ikiwepo sekta ya kompyuta na usalama wa mitandao ambapo pamoja na kufanya shughuli za kibiashara pia tunalenga kukuza uchumi wa kidijitali baina yetu na nchi zingine, kwa hapa Tanzania tutafanya kazi kulingana na mahitaji,” amesema Zhaoping.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga amesema pamoja na mambo mengine, pia wamekubaliana kuvutia kampuni mbalimbali za Kielekroniki kuwekeza nchini ambapo mwaka 2025 kutakuwa na maonesho makubwa ya utengenezaji wa vifaa vya kompyuta Afrika ambapo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume ya TEHAMA watakuwa wenyeji wa maonesho hayo.