Utindio wa Ubongo
Ni tatizo la mfumo wa fahamu (Neurologia), unaohusisha ubongo na mfumo wa neva za fahamu, ambalo huathiri sehemu ya ubongo inayohusika na misuli ya mwili na hutokea iwapo Ubongo haujakamilika katika ukuaji wake au kupata shida wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.
Mara nyingi watu huhusisha tatizo hili na mambo ya kishirikina, mfano watu husema wazazi wamefanya hivyo ili kujitajirisha kitu ambacho sio kweli, na wengi wamepoteza pesa na mali kwa waganga na hata uhai wa Mtoto kutokana na kutozielewa njia sahihi za kuwaokoa.
Sababu za tatizo.
Kuna sababu nyingi za mtindio wa ubongo, ikiwemo
i. Maambukizi anayopata mama wakati wa ujauzito
ii. Kupata matatizo wakati wa kujifungua kama kumbana mtoto au kutumia mda mrefu wakati wa kujifungua au kujifungua kabla ya wakati( premature birth).
iii. Kutokwa kwa damu kwenye Ubongo wa mtoto.
iv. Kubadilika kwa mfumo wa vinasaba(genes) ambazo zinaweza kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.
Dalili.
Dalili za matatizo ya akili huonekana sana katika kipindi cha umri wa miaka mitatu ya mwanzo ya ukuaji baada ya kuzaliwa, kama ifuatavyo:
i. Kukaza kwa misuli au misuli ya mwili kushindwa kufanya kazi (hypotonia).
ii. Kulegea au kuishiwa nguvu kwa misuli.
iii. Kutokuwa na uwezo wa kuuzuia na kuufanya mwili anavyotaka (balance and co-ordination problem).
Dalili hizi zinaweza kuonekana sehemu mbali mbali za mwili na inategemea na kiasi gani umeathiriwa na tatizo hili, Watoto wengine wanaweza kuwa na matatizo madogo madogo, ila wengine hupatwa na ulemavu.
Athari.
Watoto wengi wenye mtindio wa ubongo huwa wanapata matatizo mbalimbali iikiwemo yafuatayo:
i. Kifafa katika ukuajia.
ii. Kushindwa kutafuna na kumeza chakula.
iii.Kutoweza kuongea.
iv Kupata choo kigumu au kwa shida (constipation).
v. Kutoweza kuzuia mkojo kutoka.
vi. Matatizo ya kuona na kusikia.
vii. Matatizo ya kiunzi (skeleton), kama kupinda kwa uti wa mgongo (curved spine).
viii. Mifupa kukaa sehemu tofauti kama mfupa wa paja (hip dislocation).
Utambuzi.
Mengi yanasemwa kuhusu athari za tatizo la utindio wa ubongo kwa watoto, hali ambayo imekuwa ikisababisha jamii mbalimbali kuwanyanyapaa na hata kuwabagua, lakini waweza mtambua mwenye tatizo hili kwa dalili zifuatazo:
i. Mtoto kuchelewa kukua kama watoto wengine.
ii. Mtoto kuchelewa kukaa au kukaza shingo vizuri,
iii. Viungo kukakamaa mara kwa mara au kulegea kupita kiasi.
Ushauri.
Kimsingi, tatizo hili ni uwezo wa ubongo kutokukua vizuri na kushindwa kufanya kazi yake katika mazingira yake ya kawaida. Mtu mwenye uwezo mdogo wa kufikiri, si kwamba ana matatizo ya akili ama mtindio wa ubongo. Mtindio wa ubongo unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo ubongo kuathirika wakati wa kuzaliwa, na hata maisha ya utotoni.
Wapo watoto wengi ambao wana tatizo hili na hata wazazi wao wamekata tamaa kabisa mara baada ya kuhudumiwa katika Hospitali au Vituo vya Afya bila Mafanikio, kiasi wengine wameenda mpaka kwa waganga wapiga ramli na baadhi ya watoto wamelemaa na wengine kupoteza maisha.

Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Emory cha Atlanta, Marekani katika Kitivo cha Dawa, unabainisha kuwa baadhi ya watoto wenye mtindio wa ubongo wanafundishika, wanaweza kubadilika, iwapo tu watafundishwa kwa makini na utulivu.

Mtu anayemfundisha mtoto wa aina hii, inashauriwa kuwa hatakiwi kuwa na hasira na pia inashauriwa kuwapongeza wanapofanya vizuri japo kidogo na zaidi Watoto wa aina hii inatakiwa wapewe nafasi ya kujenga urafiki na watoto wenzao wa rika lao, wasitengwe, wachanganywe na Wanafunzi wenzao wasio na matatizo ya akili, utaratibu unaojulikana kitaalamu kama ‘mainstreaming’.

Dkt. Biteko: Tanzania kujifunza Teknolojia ya Magari Singapore
Utamaduni unavyowaheshimisha Wamakonde