Moja ya malengo ya Kongamano la Kimataifa la Jotoardhi (ARGeo-C10) linalofanyika nchini Tanzania ni kuwezesha Afrika kuongeza kasi ya uendelezaji wa rasilimali ya Jotoardhi, ambayo ikiendelezwa ipasavyo barani Afrika itaweza kutumika kwa namna mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme pamoja na matumizi mengine ya moja kwa moja kwenye Sekta ya Kilimo na Ufugaji.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio jijini Dar es Salaam katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya Jotoardhi kwa washiriki wa Kongamano la Kimataifa la ARGeo-C10 linaloendelea jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya programu za kongamano hilo.
Amesema, “Tanzania ina maeneo mengi yaliyotambuliwa yenye viashiria vya Jotoardhi na tayari Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC) inaendelea na shughuli za utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwemo Songwe, Kiejo-Mbaka na Ngozi.”
Dkt. Mataragio ameongeza kuwa, kwa Tanzania kuweka mkazo kwenye uzalishaji wa umeme kwa kutumia chanzo cha Jotoardhi kunaendana na malengo ya dunia ya kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa kwani Jotoardhi ni nishati safi.
Amesema mafunzo yaliyotolewa katika Kongamano la Kimataifa la ARGeo-C10 kuwa ni pamoja na uendelezaji wa mashapo ya Jotoardhi na teknolojia mpya, Matumizi ya moja kwa moja ya jotoardhi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji hasa wa samaki pamoja na athari za masoko ya kaboni (carbon markets).
Nchi mbalimbali zilizoshiriki mafunzo hayo zinazojihusisha na rasilimali ya Jotoardhi ni pamoja Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Nigeria, Cameroon na New Zealand ambapo Tanzania imeweza kupata uzoefu kutoka nchi nyingine zilizopiga hatua kubwa katika uendelezaji wa nishati hiyo.