Wakala wa Usajili wa Biashaa na Leseni (BRELA), imeandaa Mkutano wa Pili wa BRELA na Wadau wakee, utakaofanyika Oktoba 25, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari hii leo Oktoba 23, 2024 imeeleza kuwa mkutano huo ni wa pili kufanyika ambapo utawakutanisha wadau mbalimbali kutoka Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, kwa lengo la kujadili fursa, mafanikio na changamoto zinazowakabili wadau wa BRELA na Sekta ya Biashara kwa ujumla.
Aidha, mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano baina ya BRELA na wadau wake kutoka Sekta ya Umma na Binafsi ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA na Taasizi zingine zinazoratibu urasimishaji wa biashara nchini.
“Kauli mbiu ya Mkutano huu ni, Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation). Kauli Mbiu inakwenda sambamba na maagizo na maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mifumo inasomana ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu,” ilieleza taarifa hiyo.
Pia, kwa kuwa urasimishaji wa biashara ni mchakato, BRELA imeeleza kuwa ni vyema kupitia Mkutano huu Sekta za Umma zinazoratibu urasimishaji wa Biashara nchini wakasikiliza namna bora ya Sekta Binafsi inavyopenda ihudumiwe kupitia mifumo kusomana.
Imesema, “kutokana na uzoefu uliopatikana katika Mkutano wa kwanza wa wadau wa BRELA uliofanyika Oktoba 27, 2023 na kuhudhuriwa na washiriki wapatao 350, ulitoa mwanga na kuonesha umuhimu wa kukutana na kukaa pamoja na wadau kila mwaka, ili kubaini fursa, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo sekta binafsi.”
Kupitia Mkutano huo, wadau wataweza kupata mrejesho wa majukumu yanayofanywa na BRELA ikiwemo kupata mrejesho wa maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau kwenye Mkutano wa wa BRELA na Wadau wake uliofanyika mwaka jana 2023.
Pia utajadili mada kuhusu mifumo ya Taasisi za Serikali kusoma na uwezeshaji kibishara nchini, kupata mrejesho wa huduma za BRELA na kuweka mkakati wa pamoja, ili kuboresha huduma zinazotolewa, kupata maoni juu ya utendaji kazi wa BRELA hasa matumizi ya mifumo kwa kusomana na mifumo ya Taasisi zingine, kubaini changamoto zinazowakabili wadau na kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Aidha utajadili pia kukuza uelewa wa wadau kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utoaji wa huduma za usajili, ulinzi na utoaji Leseni, ili kuimarisha utekelezaji wa sheria za nchi, na ujadili masuala yanayohusu maendeleo ya Sekta ya Biashara nchini ikiwemo fursa zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia na namna yanavyochochea ukuaji wa biashara.
Mkutano huo wa Pili wa BRELA na Wadau wake utawakutanisha wadau zaidi ya 300, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za umma, sekta binafsi, Taasisi miamvuli, wafanyabiashara, wanazuoni, wajasiriamali na Mawakili kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Aidha mkutano huo pia, utakuwa sehemu ya kubadilishana uzoefu utakaowezesha kuboresha na kuimarisha huduma pamoja na kuongeza ufanisi na tija kwenye utoaji wa huduma na utasaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo wateja na wadau wa BRELA.
Taarifa hiyo imezidi kufafanua kuwa pia utaendeshwa kwa muundo wa Mdahalo ambao utawezesha watoa mada, wachagizaji na waongoza mijadala kuhusiana na mada zilizopo kuibua mjadala kulingana na mada husika pamoja na kauli mbiu ya Mkutano huu wa pili. Kauli mbiu hii, itatumika katika kuakisi mada zitakazo tolewa kwa kuzingatia ushiriki wa wadau waliopo kwenye mnyororo mzima wa urasimishaji na ufanyaji wa biashara nchini.
Washiriki wapatao 300 wanatarajiwa kushiriki katika Mkutano huu ambapo Taasisi mbalimbali zimeonesha nia ya kushiriki katika Mkutano kama washiriki na baadhi wakiwa sehemu ya wadhamini.