Mkazi wa Kata ya Rwamishenyi Manispaa ya Bukoba, ambaye pia ni Daktari wa Viungo, Haruna Ayubu maarufu kama Rubai (63), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Bukoba akikabiliwa na shitaka la ubakaji wa mtoto wa miaka 12.

Kesi hiyo ya jinai namba 30251/2024, inasimamiwa na Mawakili wawili wa upande wa mashitaka ambao ni Matilda Assey pamoja na Alice Mutungi na katika maelezo ya awali ilidaiwa kati ya Desemba 2023 na Oktoba 19, 2024 mshitakiwa amekuwa akimuingiza mhanga katika moja ya chumba cha ofisi yake iliyopo mtaa wa Pwani, Kata ya Miembeni.

Wakili Assey alisema, alipoingia katika chumba hicho alimvua mhanga nguo na kumtendea tukio hilo na amekuwa akimpatia shilingi 10,000 au 5,000 kwa ajili ya kuwapelekea wazazi wake na Oktoba 19, mwaka huu mhanga alikwenda tena katika ofisi ya mshitakiwa kwa lengo la kuchukua fedha ambayo amekuwa akimpatia kama msaada baada ya tukio la kumuingilia kimwili.

Amesema, “mhanga alipotoka katika chumba hicho ndipo alitokea askari polisi na kumuhoji mhanga ndipo mshitakiwa aliweza kukamatwa na kisha kupelekwa kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano. Mhanga alipelekwa hospitali na Daktari alithibitisha kuwa ni kweli aliingiliwa na upelelezi wa shauri hilo umekamilika tupo tayari kuendelea na kesi, tuna mashahidi 10, vielelezo vya maandishi vitatu na ripoti ya daktari.”

Wakili wa upande wa utetezi, Frank John aliieleza Mahakama hiyo kuwa hawako tayari kuendelea na kesi na kudai kuwa ili mshtakiwa aweze kusikilizwa kikamilifu lazima awe amepewa maelezo ya mlalamikaji kwani pamoja na kusomewa shitaka bado mshitakiwa hajapewa hati ya mashtaka na hoja ya tatu apate muda wa kuongea na mteja wake, ili aone ni jinsi gani ya kuweza kumtetea katika shtaka linalomkabili na ndiyo msingi muhimu wa haki ya kuwakilishwa na wakili.

Aidha, aliiomba Mahakama kuahairisha shauri hilo kwa tarehe nyingine ambayo watakubaliana pande zote mbili kwani siku moja kabla ya kesi hiyo alipata msiba wa kufiwa na kaka yake.

Akijibu hoja za Wakili wa upande wa utetezi, Wakili wa Serikali Alice Mutungi alisema mshitakiwa alifikishwa Mahakamani tangu asubuhi hadi saa kumi jioni kama alitaka kuongea na mteja wake wangekuwa wameshaongea na kuiomba mahakama kuangalia maslahi ya mtoto ambaye ni mhanga katika shauri hilo, ambaye pia amekuwepo Mahakamani tangu asubuhi kwa ajili ya kusikilizwa.

“Tukisema shauri hili lihairishwe mtoto aondoke na kurudi tena tunaona kwa mazingira haya sio salama kwa mtoto,tunaiomba mahakama yako tukufu kwa maslahi ya mtoto shauri hili lisikilizwe kwa haraka ili mtoto asiwe anakuja mahakamani na kurudi, hati ya mashtaka alipewa Wakili wa mshitakiwa na Wakili hajakana amekiri kupokea hati hiyo kisheria wakili ni muwakilishi wa mshitakiwa na yupo kwa ajili ya kumsemea.” alisema wakili Alice.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Andrew Kahabuka baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, aliwataka upande wa utetezi kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni wadhamini wawili wakazi wa manispaa ya Bukoba wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya Shilingi Milioni nne kila mmoja.

Aidha, Mtuhumiwa alitakiwa kutotoka ndani ya Manispaa ya Bukoba isipokuwa kwa kibali maalum cha Mahakama na baada ya kutimiza masharti hayo alidhaminiwa huku kesi yake ikitarajiwa kutatajwa tena Oktoba 19, 2024 lakini hata hivyo alikamatwa tena akiwa amefika nyumbani kwake.

Mfupa uliomshinda Zahera wakabidhiwa kwa Mgunda
Msiwakwamishe Wajasiriamali wadogo - Kigahe