James K. Mwanamyoto, OR-TAMISEMI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amevitaka Vyama vya Siasa Nchini kuhamasisha Wanachama wao kujitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ili wananchi waweze kuwa na uwanja mpana wa kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo kwenye maeneo yao.
Mchengerwa ametoa wito huo kwa vyama vya siasa wakati akitoa takwimu za wananchi waliojiandisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo ya TAMISEMI jijini Dar es Salaam.
Amesema, “nitoe rai kwa vyama vyote vya siasa kuendelea kuwasihi wanachama wao kudumisha amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kulinda amani, utulivu na ustawi wa nchi yetu.”
Aidha, Mchengerwa amevitaka vyombo vya dola kuhakikisha kuwa kuna na amani na utulivu wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea ili wananchi wote waweze kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu na kuwasisitiza wasimamizi wa uchaguzi na wadau wote wa uchaguzi kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi ili mchakato uwe wa huru na wa haki na hatimaye wananchi wote wenye sifa waweze kushiriki.
“Hakikisheni wagombea wote wanahudumiwa vizuri wakati wa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu na hakikisheni vyama vyote vimepata maelekezo sahihi kuhusu uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi za uongozi,” alihimiza Mchengerewa.
Novemba 27, 2024 ndiyo siku ambayo Watanzania 31,282,331 waliojiandikisha watapata fursa ya kuwachagua Viongozi wa Serikali za Mitaa nchini.