Boniface Gideon, Pangani – Tanga.
Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, wamekabidhi rasmi fedha Shilingi Milioni 10.5 kwa Wakazi wa Kijiji cha Sange kilichopo Kata ya Mkwaja wilayani Pangani, zitakazosaidia kuongeza wigo wa ajira kwa jamii yao ambayo uchumi wake unategemea shughuli za Uvuvi wa Samaki na Kilimo.
Mratibu wa Mipango wa Shirika hilo, Abubakari Massoud aliwaeleza Wakazi wa Kijiji hicho wakati wa hafla ya kukabidhi fedha kuwa Shirika hilo limekuwa likitoa fedha na vitendea kazi, kwa vikundi na Wakazi wanaoishi ukanda wa Bahari, ili wapunguze shughuli Baharini kwa lengo la kutunza mazingira na kuongeza uzarishaji wa Samaki.
Amesema, “tumekuwa na utaratibu,wakutoa fedha na vitendea kazi kwa vikundi na Wakazi wanaoishi ukanda wa Bahari ili wapunguze shughuli za kiuchumi majini,shughuli zote hizi,tunazifanya ili kuisadia jamii yetu na kunusuru Viumbe Bahari, tutaendelea kuwasaidia pale ambapo mnahitaji Msaada.”
Abubakari ameongeza kuwa, “jumla ya vikundi 5 vyenye Wanachama 150 katika Kijiji hiki,tumewakabidhi fedha hizi ili wakaendeleze Biashara zao , kabla ya kukabidhi fedha hizi,tumewapatia mafunzo ya ujasiriamali na kuwajengea uwezo wa kusimamia fedha,tunaamini kuwa fedha hizo zitasaidia kuongeza ajira kwa jamii nzima na shughuli za kiuchumi Baharini zitapungua.”
Kwa upande wake Msimamizi wa Idara ya Kilimo na Uvuvi, Halmashauri ya Wilaya Pangani, Ramadhan Zuberi aliwataka Wakazi wa Kijiji hicho pamoja na wanufaka wa fedha hizo,kutumia vizuri na kusema, “Fedha hizi tunatarajia kuwa zitaenda kuzaa zaidi,nimeona, kwenye Kata na vijiji ambavyo walianza kupata tayari wamefanya vizuri, kwenye Kijiji cha Bweni wameshafikisha Milion 40 ndani ya Muda mfupi,hivyo jitahidini na nyie tuone mafanikio makubwa.”
“Tunawaomba Mwambao Coastal Community Network Tanzania,mtusaidie Boti ya doria,kwa Wakazi wa Kijiji hiki wamepata Elimu ya mazingira na Ulinzi, lakini huko Baharini tunachangamoto ya mwingiliano kutoka kwa wavuvi wa nje ya Kijiji hiki, kwahiyo tukipata Boti itatusaidia sana kwenye Ulinzi,” aliongeza Zuberi.