Chama cha waandishi wa habari wa wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) wameongeza muda wa wanahabari kwenye kuwasilisha kazi zao kwaajili ya ushiriki wa tuzo za Samia Kalamu Awards.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam mkurugenzi mtendandaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema uamuzi wa kuongeza muda umefanyika ili kutoa nafasi kwa wale waliokutana na changamoto za kiufundi ikiwemo kushindwa kupandisha kazi mtandaoni kutokana na changamoto ya mtandano.
Dkt. Reuben amesema lengo la tuzo hizo ni kuhamasisha, kukuza na kupanua wigo wa wa uandishi, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari vya asili na mtandaoni ili kuchochea uandishi wa makala za kina zinazozingatia maendeleo, uwajibikaji, mila na tamaduni pamoja na kujenga chapa ba taswira ya nchi yetu.
“Kwa taarifa hii tunawatia moyo wale ambao bado hawajawasilisha kazi zao kuchukua hatua haraka na kufanya hivyi kabla ya tarehe mpya ya mwisho.
“Pia tunapenda kuwakumbusha kuwa kazi zinazowasilishwa zinatakiwa kuwa za kipekee na ambazo hazijawahi kuwasilishwa kuwania tuzo nyingine na zinazofuata taratibu rasmi na za haki miliki na waandishi wanatakiwa kuwasilisha kazi zai kupitia tovuti rasmi ya ya tuzo ambayo ni www.samiaawards.tz na taarifa zaidi zinapatikana kwenye tovuti hii,” amesema Dkt. Reuben.
Mchakato wa upigaji kura kwa wananchi utaanza rasmi tarehe 08 Novemba 2024 huku wanahabari wakihimizwa kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika upigaji kura kwani wananchi huchangia kura zao kwa 60% ya alama za mshindi huku 40% zikiamuliwa na jopo la majaji pia wananchi wataweza kushiriki kupiga kura kwa namba maalumu ya SMS SHORT CODE 15200 au kwa kutumia tovuti rasmi ya tuzo.
Ikumbukwe mnamo Oktoba 13, 2024 tuzo hizo zilizinduliwa rasmi zikiwa na kauli mbiu ya UZALENDO NDIO UJANJA na baada ya hapo muda wa ushiriki wa tuzo hizo umesogezwa mbele hadi Oktoba 30, 2024.