UPIMAJI NA MATIBABU YA MOYO BILA MALIPO KLINIKI YA JKCI KAWE

WANAHABARI KUPEWA KIPAUMBELE

 

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Peter Kisenge wanatarajia kutoa huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Kupitia taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Wizara ya Afya, Anna Nkinda imeeleza kuwa huduma hiyo itatolewa bila malipo kwa watoto na watu wazima wakiwemo Waandishi wa Habari, lengo likiwa ni kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo karibu zaidi na wananchi.

Matibabu hayo yatatolewa Oktoba 29-30, 2024 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika Kliniki ya JKCI Kawe iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari.

Aidha, taarufa hiyo pia imeeleza kwamba kutakuwa na Wataalamu wa lishe watakaotoa elimu ya lishe bora itayayowapa Wananchi uelewa wa kufuata mtindo bora wa maisha na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo yanayoweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

“Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupima afya zenu kujua kama mna matatizo ya moyo ili kuanza matibabu mapema kwa atakayegundulika kuwa mgonjwa,” ilieleza taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo imewataka wale ambao watajitaji maelezo zaidi kuwasiliana kwa simu namba 0783922571 na 0680280007 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya Kawe.

Maisha: Jamani nyie acheni, uchawi wa mapenzi upo
Taasisi za Nishati zahimizwa ushirikiano, Ubunifu