Watendaji na Watumishi katika Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati wametakiwa kuwa na umoja, ushirikiano na ubunifu ili kusogeza huduma bora kwa wananchi ikiwemo za umeme, mafuta na Nishati Safi ya Kupikia.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko jijini Dodoma wakati wa Kikao chake na Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake ambacho ni cha pili kutoka uanzishwe mfumo mpya ndani ya Wizara na Taasisi zake wa kujifanyia tathmini ili kuona namna inavyofanya kazi ya kuhudumia wananchi.
Katika Kikao hicho, Dkt. Biteko amewataka watendaji wa Wizara na Taasisi kufanya kazi kwa bidii na weledi huku wakimuangalia mtanzania wa kawaida anayetegemea mipango ya Serikali ili kuweza kubadili maisha yake na kukumbuka kuwa Sekta ya Nishati ni injini ya uchumi wa nchi hivyo inapotetereka yanatokea matatizo kwenye nyanja zote za kiuchumi na hali ya maisha ya watu.
Vilevile amewakumbusha watendaji wa Wizara na Taasisi kutochukua muda mwingi kulinda vyeo bali kinachotakiwa ni matokeo ya kazi zitakazoacha alama kwenye Taasisi kwani vyeo huwa havidumu.
Pamoja na kupongeza Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi, ametaka kila Taasisi kuwa na Vigezo vya Upimaji wa Utendaji Kazi vitakavyotumika kufanya tathmini ya uelekeo wa Sekta ya Nishati nchini.
Dkt. Biteko amewasisitiza Watumishi wote kutenda zaidi kuliko kusema, kujenga taasisi imara kuliko mtu imara na kujenga Sekta ya Nishati imara kuliko Waziri imara ili kuweza kuwahudumia wananchi vizuri na kwa haraka.
Aidha, ameagiza Watendaji kueleza mafanikio ya Sekta ya Nishati kwa watanzania.