Kamati ya Bunge Nchini Kenya, imekataa pendekezo la Rais William Ruto la kutaka kufanyia marekebisho katiba na kuundwa kwa Ofisi ya Kiongozi wa Upinzani, wakisema hatua hiyo itadhoofisha mfumo wa Serikali.
Hatua hiyo, pia imeungwa mkono na baadhi ya Wanachama wa Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria – JLAC, hasa wa ODM, ambao nao walikataa pendekezo la kufanyia marekebisho katiba, ili kuunda afisi ya Waziri Mkuu.
“Mfumo wa utawala ni wa urais. Kifungu cha 108 cha katiba kinatoa nafasi kwa viongozi wa vyama katika Bunge la Kitaifa na wanajumuisha kiongozi wa chama cha wachache ambaye kimsingi ndiye kiongozi wa upinzani bungeni,” ilifafanua ripoti ya JLAC.
Wakati huo huo, mizozo ya kisiasa kati ya Magavana na Wawakilishi wa Wadi, imedaiwa kutatiza shughuli na kukwamisha miradi muhimu katika kaunti mbalimbali, baada ya Magavana na Mawaziri wa Serikali zao kutimuliwa ofisini na kusababisha kaunti kushindwa kutoa huduma kwa Wananchi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya hivi karibuni, miradi ya thamani ya Shilingi Milioni 673.7 imetatizoka na mingine kutokamilika katika Kaunti mbalimbali.