Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa kipaumbele kwenye ujenzi wa miradi ya nishati jadidifu nchini ili kusaidia utunzaji wa mazingira, kuzalisha umeme wa uhakika na kutoa ajira kupitia miradi hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Teknolojia Mbadala na Nishati Jadidifu kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alipotembelea mradi wa Mwenga Hydro unaozalisha umeme wa maji wa megawati nne katika Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.
Amesema, “sisi kama wakala tunaendelea kufadhili hii miradi kwa kuhamasisha na kuwawezesha wanaojenga miradi ili kuendeleza shughuli za kiuchumi nchini.”
Awali, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mwenga Hydro, Deograsias Massawe alisema mradi huo umewezesha wananchi wa vijiji 32 vya Wilaya ya Mufindi kupata umeme wa uhakika hivyo, kuwawezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Alisema, mradi huo umekuwa na faida kwa wajasiriamali kwa kutoa ajira na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ambao umepunguza gharama za uendeshaji shughuli za kiuchumi kutokana na kuachana na matumizi ya mafuta na kuhamia kwenye matumizi ya nishati ya umeme.
Aidha, ameipongeza REA kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 16.6 ambazo zimefanya maunganisho kwa wateja zaidi ya 8000 wa majumbani, hospitalini, mashuleni na kwenye vituo vya afya ambapo Mradi huo umeanza uzalishaji rasmi mwaka 2012 katika Wilaya ya Mufindi na umelenga kuongeza wateja wapatao 2,900 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.