Mkurugenzi Mtendaji wa Dar24 Media na Mfanyakazi wa Kampuni DataVision International Limited, Maclean Godfrey Mwaijonga, ambaye aliripotiwa kupotea Oktoba 31, 2024 amepatikana.

Akiongea mbele ya Wanahabari, Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amesema Mwaijonga amepatikana Kigamboni akiwa katika hali ya kutokua na nguvu ambayo inatokana na kunywa kinywaji kinachosadikika kuwa na kitu kilichopoteza fahamu zake.

Amesema, “jioni ya leo tumepokea taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu kuwa Mwaijonga ameonekana Kigamboni, tukaongozana na familia mpaka huko Buyuni na kumkuta akiwa hana nguvu, tukampeleka Hospitali tunashukuru hana tatizo. Lakini anasema alikua na watu anaowafahamu kwa mazungumzo ya biashara.”

Akihojiwa kuhusu uhalisia wa tukio, Maclean amesema alikutana na watu ambao walikuwa kijadili jambo kuhusu mambo ya kibiashara na walielekea Kigamboni akiwa anaendesha gari yeye mwenyewe.

“Nilipofika kule tulikaa nikaagiza ‘Juice’ (Sharubati) na nilipokunywa nilipoteza fahamu, ni watu ninaowafahamu na hata nilipozinduka walikuwa wakiniuliza maswali kuhusu biashara na baadaye walinizungusha tukiwa wote ndani ya gari,” alisimulia Maclean.

Dar24 Media na Kampuni ya Datavision International inatoa shukrani za dhati kwa Vyombo vyote wa Habari vilivyoungana pamoja katika kupaza sauti kuutaarifu umma juu ya kupotea kwa Mkurugenzi wetu Maclean.

Taarifa zaidi kuhusu kupatikana kwake tembelea YouTube Channel ya Dar24 Media.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Novemba 3, 2024
Muliro: Tunafuatilia, tunachunguza kupotea kwa Maclean Mwaijonga