Usonji ni tatizo linalojitokeza mapema utotoni, ambapo mtoto huwa na mapungufu kwa kupenda kujitenga na kutotaka kuwa karibu na watuhupata matatizo ya lugha na shida ya mawasiliano na huwa na tabia ya kurudia rudia kitu anachokifanya mara nyingi.

Usonji kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani – WHO, humkumba mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 ulimwenguni wakisema tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea..

Chanzo halisi cha tatizo hili la usonji hakijulikani ingawa  matatizo ya kijenetiki yanahusishwa ikidaiwa kuwa maambukizi ya Rubella au matumizi ya pombe na dawa za kulevya aina ya coccaine wakati wa ujauzito au sababu za kimazingira, husababisha tatizo la usonji.

 

Wataalamu wanasema ni aghalabu kuona dalili hizo ambapo zinapojitokeza mtoto hukosa mbinu za uhusiano, anashindwa kuzungumza na wakati mwingine kurukaruka na hata kujing’ata.

Watoto wa kiume huathirika zaidi ikilinganishwa na watoto wa kike ambapo kwa kila watoto watatu wa kiume wenye kupata usonji ni mtoto mmoja tu wa kike anaepata maradhi hayo na kutokana na tatizo hilo wengine hutelekezwa na jamii na kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa. .

Jarida la The Lancent la mwaka 2013, linasema watu wapatao milioni 21.7 wameathirika  kwa tatizo hili la usonji  ulimwenguni kote na inaelezwa kuwa tabia za kujirudia rudia kwa mtoto aliyeathirika na tatizo la usonji zimegawanyika katika makundi yafuatayo,

  • Tabia zilizozoeleka – Kama  kupiga piga mikono, kutikisa tikisa kichwa mara kwa mara na kujibiringisha mwili
  • Tabia ambazo huchukua sana muda kama za kupanga panga vitu kwa mpangilio maalum au kuosha mikono mara kwa mara
  • Tabia ya kung’ang’ania vitu visihamishwe kwa mfano viti au kutokubali kukatizwa katizwa

Ugunduzi.

Ugunduzi wa tatizo hili la usonji hufanyika kwa

  • Daktari wa watoto  kumpima vipimo vya kawaida pamoja  na kuchukua historia ya  ukuaji wa mtoto husika.
  • Daktari bingwa wa watoto aliyebobea kwenye matatizo ya kisaikolojia ya watoto kumpima ili kuangalia tabia za mtoto. huyu  na uwezo wake wa kiakili.
  • Vipimo vya kijenitikia hufanyika baada ya kugundulika kwamba chanzo cha  tatizo la usonji ni matatizo ya kijenetiki.

Kadri mtoto anavyoendelea kukuwa ndio usonji unavyoweza kutambulika kwa urahisi zaidi kwani madhara yake yanaonekana kwa urahisi wakati wa  ukuaji wa kiakili wa mtoto.

Uchunguzi.

Mchunguze mtoto wako kwa viashiria vya tatizo la usonji mapema zaidi kwani kumchelewesha mtoto mwenye usonji kupimwa na kupewa tiba mapema huchangia tatizo hili kuwa kubwa zaidi na hivyo kuathiri matokeo ya matibabu ya tatizo hili.

Nusu ya wazazi hugundua watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya miezi 18 ya umri wa mtoto, na moja ya tano ya wazazi hugundua ya kwamba watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya kipindi cha miezi 24 ya umri wa mtoto na tabia hizi ambazo si za kawaida katika ukuaji wa mtoto ni.

  • Kutotamka maneno ya kitoto  mpaka anapotimiza umri wa mwaka mmoja.
  • Kushindwa kuotesha kidole au kumpungia mzazi au mtu yoyote mkono mpaka anapotimiza umri wa miezi 12
  • Kushindwa kutamka neno lolote mpaka anapotimiza umri wa miezi 16.
  • Kutotamka maneno mawili kwa pamoja au sentensi mpaka umri wa miezi 24.
  • Kupoteza uwezo wa kuongea au kutokuwa na tabia ya kutangamana/kuchanganyikana na watu wengine wakati wowote ule katika umri wa mtoto.

Matibabu.

Familia yenye mtoto mwenye tatizo la usonji huhitaji kuelemishwa jinsi ya kuishi na mtoto huyo pamoja na kusaidiwa katika malezi yake. Kwa kuwa tatizo hili  halitibiki ni muhimu mtoto kupata.

  • Tiba ya Tabia
    • Uchambuzi wa tabia : Kutumia utaalamu wa kisaikolojia kufundishia na kuwahusisha na jamii, kuboresha mawasiliano, na usimamizi wa kitabia
    • Matibabu na elimu ya usonji kwa kuboresha mawasiliano kwa watoto wenye ulemavu
  • Tiba nyingine muhimu ni kuelimisha jamii kuhusu watoto wenye usonji , jinsi ya kuishi nao na kuwaanzishia watoto wenye usonji matibabu mapema.

Hata hivyo, katika siku yaKimataifa ya usonji Duniani Aprili 2 Umoja wa Mataifa ulitaka elimu zaidi itolewe, ili jamii ibadili mtazamo ikisema watoto wenye usonji wakipatiwa huduma mapema wanaweza kushiriki vyema katika jamii zao kwani wana uelewa wa hali  ya juu.

Hizi hapa mechi zinazopigwa leo Ligi kuu NBC
PSG :Ufalme wa Mbappe umechukuliwa na nyota hawa