Mimba za utotoni ni ujauzito anaoupata Mwananmke aliye chini ya umri usiofaa katika jamii fulani, ambazo zinahusishwa na masuala ya kijamii, ikiwa ni pamoja na viwango vya chini vya elimu na umaskini.
Tatizo hili la mimba za utotoni limekuwa kubwa duniani na linaongezeka siku hadi siku hasa katika jamii ya uchumi wa chini huku sababu zinazopelekea jamii ya uchumi wa chini kukumbwa sana na tatizo hilo ni ukosefu wa taarifa za afya ya uzazi na umasikini.
Tanzania inaendelea na mapambano dhidi ya mimba za utotoni, ingawa bado kuna changamoto, tukikumbuka kwamba Oktoba 28, 2023 wakati akizungumza katika uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na viashiria vya Malaria Rais Samia mikoa inayoongoza mimba za utotoni ni Songwe asilimia 45, Ruvuma asilimia 37, Katavi asilimia 34, Mara asilimia 31 na Rukwa asilimia 30.
Ripoti ile ilionesha kumekuwa na mafanikio katika kupunguza mimba za utotoni kwa asilimia 5 kutoka asilimia 27 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 22 mwaka 2022 lakini tukilitizama tatizo hili kwa upande wa pili mbali na umasikini ama hali ya kiuchumi ni wazi kuna mporomoko pia wa maadili.
Ripoti ya hali ya idadi ya watu mwaka 2013, ambayo ilitolewa na Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu katika Umoja wa Mataifa, UNFPA, iliwahi kueleza kwamba kila mwaka, watoto milioni 7.3 wa kike chini ya umri wa miaka 18 hushika na kujifungua mimba.
Ripoti hiyo, ilisema kati ya watoto hao milioni 7.3 milioni mbili wana umri usozidi miaka 14, ambao hukumbana na matatizo ya muda mrefu ya kiafya na kijamii kutokana na mimba hizo, ikiwemo vifo vinavyohusiana na uzazi huku wito wa kubuni mbinu za kina za kukabiliana na changamoto za mimba za utotoni ukitolewa.
Mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike. Mtoto wa kike asiye na elimu atakuwa na ugumu kupata ajira na kujijengea maisha bora na familia yake. Msichana anayeshika mimba akiwa na umri wa miaka 14 au chini yake, haki zake zitakuwa zimekiukwa.
Kuna wasichana milioni 580 duniani sasa. Ripoti ya mwaka 2023, ilionesha kuwa kwa kuwekeza kwa watoto wa kike, kuwapa nguvu, na kulinda haki zao, inawezekana kabisa kuwasaidia kufikia ndoto zao.
Zipo athari za Mimba za utotoni kubwa ni uchungu wa kujifungua kwa muda mrefu au kushindwa kujifungua kutokana na viungo vya uzazi au nyonga kutokomaa, kupata kifafa, kifo, mtoto kuzaliwa njiti, ulemavu wa kiakili au kimwili au kifo, ongezeko la watoto wa mitaani na hasara ya nguvu kazi.
Hata hivyo, Wataalamu wa afya ya uzazi wanashauri, ili kuepukana na matatizo ya kiafya ni vyema kupata mimba baada ya kufikisha umri wa miaka 18 kwani chini ya umri huo msichana anakuwa bado hajakomaa kiakili na kimwili kuweza kubeba majukumu ya malezi.
Pia nyonga huwa changa na nyembamba hivyo kutoweza kubeba kiumbe na kusababisha madhara makubwa wakati wa kujifungua.Madhara mengine ya kiafya yatokanayo na mimba za utotoni ni kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, Fistula (kutokwa na haja ndogo), kifafa cha mimba na vifo vya mama na mtoto.
Njia kuu ya kumwepusha mtoto wa kike na mimba za utotoni ni kumsomesha, hivyo jamii inatakiwa kuhakikisha mtoto wa kike anabaki shule, tukiamini kwamba kumsomesha mtoto wa kike ni kuikomboa jamii yote ikizingatiwa kwamba Serikali imefanya juhudi ya kutoa Elimu bure, hivyo ni jukumu letu kama jamii kuwapeleka watoto shuleni na kuwahimiza kusoma kwa bidii.
Tuweke pia mkazo wa kimaadili na kuishi na hofu ya MUNGU, kwa kukaa na watoto na kubadilishana mawazo juu ya faida na hasara za kukua kwa technologia, huku tukiacha lawama za mmomonyoko wa maadili na badala yake tutafute namna ya kuongea na vijana wetu waelewe uhalisia na wafuate njia iliyo sahihi kuyafikia malengo yao na kujenga kesho iliyo imara.