Tabora United yatamba dhidi ya Mashujaa FC

Klabu ya Mashujaa imeambulia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Tabora United. Huu unakuwa mchezo wa pili mfululizo kwa klabu hiyo kupoteza baada ya kufungwa bao 1-0 na Simba SC dimba la Lake Tanganyika. Matokeo hayo yanawafanya Mashujaa kusalia na alama 13 katika mechi 10 walizocheza mpaka wameteremka mpaka nafasi ya 8 kwenye msimamo wa ligi.

Ushindi wa Tabora United umeipeleka timu hiyo katika nafasi ya 7 kwenye msimamo wa ligi ikilingana na KMC wenye alama 14 wanaoshika nafasi ya 6 wote wakicheza mechi 10 na kutofautiana magoli ya kufunga na kufungwa.Huu ni mwendelezo mzuri kwa kocha Francis Kimanzi.

Maoni kwa bodi ya Ligi

Klabu ya Tabora United ilicheza mchezo wake wa raundi ya 9 Oktoba 23 na imekuja kucheza mchezo wa raundi ya 10 tarehe 04 Novemba . Hii imeonyesha kwamba Tabora United walipata wasaa wa kupumzika kwa siku 10 kuelekea mchezo dhidi ya Mashujaa.

Katika siku hizo 1o klabu ya Mashujaa ilicheza mechi 2 mchezo wa raundi ya 8 dhidi ya Fontain Gates tarehe 28 Oktoba dimba la Tanzanite Babati na mchezo wa raundi ya 9 dhidi ya Simba SC tarehe 01 Novemba dimba la Lake Tanganyika Kigoma kisha ikasafiri kuwafuata Tabora United kwa mchezo wa Raundi ya 10. Kwa tafsiri nyingine unaweza kusema ndani ya siku 8 Mashujaa wamecheza mechi 3 wakisafiri maeneo tofauti ya nchi .

Kwa mtazamo wangu ni vyema Bodi ya Ligi ikaangalia namna inavyopanga ratiba zake ili kuepusha timu chache kuumia na mpangilio huo ,ni vyema mechi zote za ligi zichezwe wikiendi ili kuwapa fursa wachezaji kupumzika vyema kuelekea mchezo unaofuata.

Kagera Sugar yarejesha ari ya ushindi 

Ushindi wa mabao 2-1  walioupata kagera Sugar dhidi ya Dodoma Jiji umewafanya kufikisha alama 8 na kusalia nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi. Hii inakuwa ni mechi ya kwanza kushinda kwa kocha Melis Medo tangu akabidhiwe timu hiyo Oktoba 17 na kuiongoza katika michezo mitatu akipoteza mechi moja dhidi ya Coastal Union mchezo uliopigwa dimba la Sheikh Abeid jijini Arusha na sare ya 1-1 dhidi ya Pamba Jiji mchezo uliopigwa dimba la CCM Kirumba.

Dodoma Jiji chini ya kocha Mecky Mexime imeendelea kusalia nafasi ya 9 wakiwa na alama 13 katika mechi 11 walizocheza.Dodoma Jiji,Coasal Union na Ken Gold ndizo Klabu zilizocheza michezo mingi zaidi ya ligi kila mmoja akicheza michezo 11

 

 

Hati Miliki: BRELA, ARIPO na WIPO wawajengea uwezo Wakufunzi
Tetesi za usajili Duniani Novemba 5