Wakala wa usajili wa Biashara na Leseni nchini – BRELA, kwa kushirikiana na Shirika la Milki Bunifu Duniani – WIPO, umewajengea uwezo Wakufunzi kuhusu masuala Hati Miliki na kulinda bunifu zao kwenye mazao mengine yanayozalishwa kwenye Viwanda na tafiti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuzifanya bunifu hizo biashara na kuziongeza thamani.
Akiongea katika Mkutano huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa ameeleza kuwa mpango huu wa kufundisha Wakufunzi umefanyika kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani WIPO, ili kuiwezesha jamii ya Tanzania kupata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya milki bunifu.
Amesema, “wengi wao uelewa wao ni mdogo, hali inayopelekea wengi wao kuwa na bunifu ambazo hazina sifa zinazohitaji kuboreshwa ili zikidhi viwango vya ubora ziwe na sifa, na nyingine zina sifa lakini hawajui wafanye nini au waende wapi ili waweze kuzirasimisha bunifu zao.”
Nyaisa ameongeza kuwa, bunifu ni ajira na pia ni biashara na zikirasimishwa zinaweza kuleta utajiri mkubwa, hivyo BRELA kwa kushirikirana na WIPO na ARIPO kwa kulitambua hilo wameona waje na mkakati wa elimu zaidi kwa jamii kupitia mafunzo wanayotoa kwa Wakufunzi ili wakafundishe wengine katika maeneo mbalimbali.
“Ni matarajio yetu kwamba elimu itafika nchi nyingi za Afrika zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi, Zambia, Botswana,Tanzania na nhi nyingine na italeta tija kubwa katika sekta ya viwanda na biashara,” aliongeza Nyaisa.
Mkutano huo wa Kimatafa ulifunguliwa na mgeni rasmi Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye ambaye alisema UDSM kimekua mwenyeji na kuwaleta pamoja washiriki nchi za Afrika wakilenga kuwapa mafunzo Wakufunzi kuhusu masuala hati miliki juu ya kulinda bunifu zao.
Amesema Chuo Kikuu cha Dar es salaam ni wabobevu katika masuala ya hati miliki kwa ngazi shahada ya uzamili na ndio sababu ya kuwa wenyeji wa mkutano huo wa Kimataifa, huku WIPO ambao ni wasimamizi wa nchi za milki bunifu wankisema nchi za Afrika zina changamoto ya kutokua na uelewa wa kutosha hivyo wameamua kutoa ufadhili na usimamizi wa mafunzo hayo.
Awali, Mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali – BPRA, Zanzibar Mohamed Ally Maalim alisema kuna umuhimu wa kuzilinda bunifu kwani nazo ni mali kama mali nyingine zinazopaswa kulindwa, ili zifanyiwe biashara na zilete faida kwa mbunifu na kukuza uchumi wa Afrika.
Mkutano huo, umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa akiwemo Outle Rapuleng wa African Intellectual Property Organisation Academy (ARIPO) na Maria Bychkovska wa Project Specialist from World Intellectual Property Organisation (WIPO).