Tanzania inatarajia kuwasilisha maandiko ya miradi mikubwa tisa ya kimkakati yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.4 katika Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) utakaofanyika
Baku, Azerbaijan kuanzia Novemba 11 hadi 22, 2024 inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema hayo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo kilichorushwa na Kituo cha runinga cha TBC1 na kutayarishwa na Ofisi
ya Makamu wa Rais.
Amesema, Ujumbe wa Tanzania utaongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo katika mkutano huo kutakuwa na majadiliano yatakayohusisha viongozi pamoja na wataalamu kutoka nchini yanayolenga
kuweka msimamo wa pamoja katika masuala mbalimbali ya hifadhi ya mazingira.
Aidha, amesema Tanzania itakuwa na banda la maonesho ambapo shughuli mbalimbali zinazofanyika nchini katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zitakuwa zikioneshwa, kwakuwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni vita ambayo nchi inaendelea kupambana nayo na kwamba inahitaji juhudi za pamoja ili kuhakikisha inafanikiwa na kuwa wananchi wanapaswa kuacha kukata miti na badala yake waipande na kuitunza.
Amesema, “Katika mkutano wa COP29 tunataka kuionesha dunia namna nchi yetu inavyohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na hivyo kutuwezesha kupata wadau ambao wataongeza nguvu katika ajenda hii na hivyo tunaweza
kupata nishati kwa gharama nafuu kwa wananchi wetu.”
Katibu Mkuu Luhemeja ameongeza kuwa nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira ambayo inaokoa miti ambayo ingekatwa ili kupata kuni na mkaa vitendo ambavyo vinaweza
kusababisha jangwa.
Kaulimbiu hii imelenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika kukuza uchumi wa taifa na kuchochea maendeleo endelevu.