Kocha Miguel Gamondi, amesema kwa sasa timu nyingi zinapokutana na Yanga zinacheza mtindo wa ‘kupaki basi’ (kukaba wakati wote), na kwamba hicho ndicho kinachosababisha kushindwa kucheza soka lao walilolizoea, kitu ambacho anakichukia.
Gamondi aliyasema hayo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa kwake yeye mfumo wake ni kushambulia na kucheza mpira wa kasi, lakini changamoto ni kucheza na timu inayokaa golini kuzuia tu.
“Tumekuwa tukikamiwa sana, napenda kucheza mpira, tuoneshane ufundi na mbinu, lakini tunashindwa pale tunapokutana na timu ambazo wao wanawaza kukaa wengi kwenye eneo lao (kupaki basi),” alisema Gamondi.
Aidha, alisema tayari ameanza kufanyia kazi mbinu zitakazowasaidia kupata ushindi mzuri wanapokutana na aina ya timu hizo zinazopaki basi.
“Tunafanyia kazi mbinu za kuhakikisha tunacheza soka letu tunapokutana na aina hizi za timu, hatuwezi kubadilisha aina ya uchezaji wetu wakushambulia na soka la kasi,” alisema Gamondi.
Akizungumzia mchezo ujao wa Ligi Kuu, alisema wamejiandaa vizuri na amehakikishiwa na wachezaji wake kuendelea kupambana kuhakikisha wanapata ushindi kwenye michezo ijayo.
“Ni lazima tusahau matokeo ya mchezo uliopita, nimezungumza na wachezaji wangu na wapo katika hali nzuri, wana hamasa kubwa, kitu kinachoniaminisha tutarejea kwenye fomu yetu ya ushindi,” alisema Gamondi.
Mechi ijao Yanga itaikaribisha Tabora United kwenye Uwanja wa Azam Complex leo, huo ukiwa ni mchezo wa kwanza tangu watoke kupoteza dhidi ya Azam FC kwa bao 1-0 katika dimba hilo.