Afarah Suleiman, Hanang’ – Manyara.
Wananchi wa vijiji vitano vya Wilaya ya Hanang, vilivyoathiriwa wa maporomoko ya udongo na tope ya Mlima Hanang’ Desemba 2023, wameomba Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini – RUWASA, Mkoa wa Manyara unaotekeleza mradi wa ukarabati wa miundombinu ya Maji, kuharakisha ujenzi huo kabla ya msimu wa mvua ili waondokane na adha ya kufuata huduma hiyo mbali.
Wananchi hao, wametoa ombi hilo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Hazali Almishi Hazali wakati akikagua utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na RUWASA Mkoa wa Manyara kwa takribani shilingi bilioni 6 zilizotolewa na mfuko wa maafa ofisi ya Waziri Mkuu.
Awali, Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara James Kionaomela ameomba Wanahanang’ kuwa na subira kwani wakandarasi wa kutekeleza mradi huo wapo kazini tayari na utakapokamilika utanufaisha wananchi 20,069 wa vijiji vya Gabadau, Kinyamburi, Sarjanda, Basodagwargwe, Gendabi na pamoja na kitongoji kimoja cha kijiji cha Nangwa.
Baada ya kujionea miradi hiyo, DC Hazali ameitaka RUWASA kuwasimamia wakandarasi walio kwenye miradi hiyo waweze kumaliza Kwa wakati.
Utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa miundombinu ya Maji iliyoharibiwa na maporomoko ya mlima Hanang’, unatarajiwa kukamilika Oktoba 2025.