Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika kuhakikisha inatoa Elimu ya Mpiga Kura kwa makundi mbalimbali katika jamii, Novemba, 2024 imetoa elimu hiyo kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) nchini katika mafunzo yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo ya siku moja kuhusu Sheria mbalimbali na Kanuni zinazoiongoza Tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani amesema elimu hiyo itasaidia kuondoa migongano baina yao na wadau wengine wa uchaguzi.
Amesema, “kimsingi hawa ndio wasimamizi wa sheria ngazi ya Wilaya kutoka Jeshi la Polisi, hivyo tumewapitisha katika Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ili iwawezeshe kuzitafsiri vyema hizi sheria na zitawawezesha katika usimamizi bora wa majukumuyao bila kuleta mtafaruku kati ya chama cha siasa au na wananchi kiujumla.”
Kailima amesema kwa sasa Polisi wanajua Wajibu wao ni nini na chama cha siasa kinatakiwa kufanya nini wakati huu ambapo Tume inaendelea na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.
Aidha, Kailima amesema wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Tume itakutana tena na Jeshi hilo na kuwapa ufafanuzi juu ya mambo mbalimbali yahusuyo Uchaguzi Mkuu ili kuendelea kuwa na uchaguzi mkuu wa amani, huru na haki na kuhakikisha baada ya Uchaguzi Mkuu hali inaendelea kuwa ya utulivu.
Kwa upande wake Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi, CP Awadhi Juma Haji amesema lengo la mafunzo hayo ni kuliweka tayari Jeshi la Polisi wakati wa mchakato wa uchaguzi na huku akibainisha kuwa Jeshi hilo ndio wasimamizi wa sheria na walinzi wa raia na mali zao.

Bungeni: Idadi kubwa ya Wahitimu hawana kazi - Kishimba
Chini ya miaka 16 marufuku matumizi mitandao ya kijamii