Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), pamoja na Tume ya Utangazaji Zanzibar zimesisitizwa kuhakikisha maudhui yanayorushwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, yanaendana na viwango vya maadili, uwajibikaji na kuhakikisha yanailinda jamii dhidi ya maudhui yenye madhara ikiwemo yanayokiuka haki za binadamu, kudhalilisha, kuchochea vurugu na chuki.

Rai hiyo, imetolewa na Kamati ya wataalamu wa masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inayoundwa na Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA- Zanzibar), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC Zanzibar) , Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) na Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC).

Usisitizaji huo, nakuja baada ya kuonekana kwa video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha wasichana wawili wakirekodiwa na kuulizwa maswali yasio na maadili na yenye kuvunja heshima na haki za binaadamu, kitu ambacho kimelaniwa vikali kufuatia uibuaji wa hisia kali kwa wadau wa habari, watetezi wa haki za binaadamu na jamii kwa ujumla na kuibua maswali yasio na majibu miongoni mwa wanahabari kuhusu maadili, haki za binadamu, na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari.

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari hii leo Novemba 8, 2024,  ZAMECO pia imeiomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar kuharakisha upatikanaji wa Sheria mpya ya Huduma za Habari nchini kwa lengo la kupunguza changamoto kama hizo kwani ukizingatia katika mapendekezo ya sheria hiyo.

“Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR 1996) Ibara (19) “Kila mtu ana uhuru wa kutoa taarifa bila ya kuathiri haki ya mtu na amani ya nchi,” hii ina maana kuwa uhuru wa vyombo vya habari unaendana na jukumu la kuheshimu utu wa kila mtu, hasa wanawake na vijana, ambao ni waathirika wa moja kwa moja katika hatari yoyote itakayotokea,” ilieleza sehemu ya Tarifa hiyo.

Aidha, wamesisitiza kuwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wa kike na jamii kwa ujumla ni ukiukwaji wa haki za binaadamu, maadili ya uandishi wa habari, na kuvuruga mipaka ya uhuru wa kujieleza ambapo unalindwa na unahitajika kwa lengo la kutoa habari sahihi na kuibua mijadala yenye tija na manufaa kwa jamii.

Hata hivyo ZAMECO imewataka wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha watoto wao wa kike juu ya thamani yao, haki zao, na nafasi yao katika jamii “ukimuelimisha mtoto wa kike ni sawa na kuielimisha jamii, sambamba na kuwaelimisha vijana wa kiume kuwaheshimu watoto wa kike kwa kuwajengea mazingira yenye maadili na heshima na kudai kuwa ipo tayari kushirikiana na wadau wa sekta ya habari na Watetezi wa haki za binaadamu kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayajirudii.

Bungeni: Idadi kubwa ya Wahitimu hawana kazi - Kishimba