Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI imeiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Kuongeza nguvu ya utoaji mafunzo ya Mfumo wa NeST ili kuzidi kujenga uwezo kwa wadau wa ununuzi nchini.
Hayo yameelezwa Novemba 8, 2024 na Mbunge wa viti Maalum kwa tiketi ya CHADEMA, Hawa Mwaifunga katika mafunzo yaliyoendeshwa na PPRA kwa wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI.
Mwaifunga amesema kuwa, Serikali imejenga mfumo wa NeST kwa nia njema ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele kupitia sekta ya Ununuzi ingawa baadhi ya watu wachache na wasiolitakia mema taifa hujificha kwenye kivuli cha kuusema vibaya Mfumo huo ili kuidhinisha nia yao ya kukwepa kutumia mfumo wa ununuzi katika michakato ya Ununuzi wa umma.
“Tunatambua kuwa mfumo huu ni mzuri na una msaada mkubwa katika kudhibiti mianya ya rusha inayoweza kujitokeza wakati wa kuendesha michakato ya ununuzi, ingawa baadhi ya watu wanaulalamikia kwa kulinda maslahi yao.
Hivyo niwaombe PPRA muendelee kutoa mafunzo haya kwa wadau wote wa ununuzi nchi kuhakikisha mnawafikia ili kukwepa lawama za kuulalamikia mfumo, maana hwenda baadhi yao hawana elimu kuhusu mfumo ndio maana wanalalamika,” alisema Mwaifunga.
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba amesema Mamlaka iko tayati kupita majimboni mwa wabunge hao kutoa elimu kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST sambamba na Sheria mpya ya Ununuzi ili kuzidi kujenga uelewa kwa wadau wa ununuzi na wananchi kwa ujumla.
“Naomba nichukue fursa hii kuwaahidi Waheshimiwa wabunge kuwa sisi kama Mamlaka tuko tayari kupita majimboni mwenu kuhakikaisha elimu kuhusu mfumo wa NeST inawafikia ili kuleta chachu na kujenga uelewa zaidi kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST,” alisema Simba.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Justine Nyamoga, kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo ameipongeza PPRA kwa kazi wanayoifanya.
Aidha aliahidi kubeba dhima ya kujenga hamasa kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo wa NeST ili kulipatia taifa thamani halisi ya fedha katika ununuzi wa Umma na hatiamae maendeleo endelevu kwa wananchi na taifa kwa ujumla.