Johansen Buberwa – Kagera.
Baadhi ya Madiwani Wilayani Muleba Mkoani Kagera, wameiomba Wizara ya Nishati kuingilia kati na kutatua tatizo la Wananchi wanaoishi kwanye Visiwa 13, ili waweze kupata huduma ya umeme ambayo hawajawahi kuipata tangu kuumbwa kwa Dunia.
Akiwasilisha swali la nyongeza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika robo ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwenye ukumbi wa Halmashari hiyo Diwani wa Kata ya Bumbire, Wenceslaus Barongo amesema changamoto hiyo imekuwa kero na tatizo kubwa kwa Wananchi wa Visiwa hivyo na kupelekea kukosa imani na Serikali yao.
Amesema, “ninatoa masikitiko yangu Mwenyekiti wa kujua mwongozo wa nchi hii kwamba kunabaadhi ya huduma katika nchi hii zinaenda kwa wananchi wa eneo furani na wengine wasipate kwenye umeme kata tano za visiwani hauwahi kusikia anachangia kuhusu huduma ya umeme wananchi wetu wameshasema serikali yetu haitujali katika swala la umeme.”
Akijibu hoja hiyo, Meneja wa Shirika la Umeme Nchini – TANESCO, Wilaya Muleba, Deo Mbuya amesema Wilaya hiyo ina idadi ya visiwa vingi na suala la jinsi gani wanaweza kupeleka umeme katika maeneo hayo linashugulikiwa na uongozi wa juu Kitaifa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashari ya Wilaya Muleba, Magongo Justus amemuomba Katibu Tawala Wilaya Muleba kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Benjamin Mwakasyege kulifikisha jambo hilo katika ngazi ya Serikali Kuu kuona ni jinsi gani Visiwa hivyo vinaweza kupata huduma ya umeme.
Kwa upande wake Diwani wa kata Mazinga, Edibil Alex ameshauri kuitafuta Kampuni ya umeme jua pamoja Madiwani wa Visiwa vyote vya Muleba waliounganishiwa na mfumo huo, ili waweze kushauriana kwani mfumo uliowekwa awali ni kandamizi kwa watumiaji.
amesema, “unit moja inauzwa kwa shilingi 3500 ukitumia ndani ya siku mbili zinakuwa zimeisha kwa Mwananchi wa kawaida upate matumizi ya mwezi mzima mpaka uwe na unit za shilingi elfu 60 na mkataba wao ni kandamizi na mtu hawezi kuwahoji jambo ambalo nikitendawili kwa wananchi wa visiwa hivyo wakati tukisubiri mpango wa Serikali.”
Jumla ya Vijiji 147 vimeunganishiwa umeme na TANESCO kati ya Vijiji 166 na Vijiji sita vipo kwa Mkandarasi anayendeleza utekelezaji na Vijiji 19 havijafikiwa na huduma hiyo pamoja na Visiwa 13 bado havijafikiwa.