Johansen Buberwa – Kagera.

Tatizo la kuzagaa kwa taka katika baadhi ya mitaa ndani ya manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, limezua sintofahamu katika kikao cha Baraza la Madiwani na kupelekea Serikali kutoa maelekezo kuwa waliokuwa wakisafisha maeneo hayo warejeshwe kazini haraka.

Akiongea katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Bilele, Sharif Tawfiq ameomba wapatiwe vibarua wa kusafisha mazingira kwenye mitaa yote kwani vibarua walio kuwepo awali walisimamishwa kazi  na mpaka sasa hawajapata mbadala wake.

Akitolea ufafanuzi wa changamoto hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mazingira Manispaa ya Bukoba, Tambuko Joseph amesema vibarua waliokuwa wakifanya kazi kwenye maeneo hayo hawaja ondelewa bali ni utaratibu wa kuwapeleka vibarua kwenye maeneo umebadilika.

Amesema, “vibarua bado wapo wanashirikiana na Kampuni ya usafi na kwa niaba ya Mkurugenzi nawasisitiza Wananchi wa maeneo hayo kwa nafasi zao washiriki kufanya usafi.”

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba, Gypson Godson amesema kwasasa hawana tarifa ya kusimamishwa kwa vibarua hao na kwenye maeneo yote yaliyotajwa hawahitaji uchafu.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kutoa maagizo kwa Kaimu Mkurugenzi na Mkuu wa Idara ya Usafi wa Mazingira kupitia baraza la madiwani kutaka vibarua hao warudishwe kazini, ili kuendelea na majukumu yao kama awali.

Mfumo wa NeST: PPRA yawafikia Watumishi wa Umma Kagera
Katibu wa CCM auawa kwa risasi, Polisi waanza uchunguzi