Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amewaagiza Mameneja wa TARURA wa Wilaya kote nchini kukagua na kusafisha madaraja na makalavati yote katika maeneo yao ili yaweze kupitisha maji kwa urahisi na kuepusha mafuriko.
Mhandisi Seff ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake katika wilaya za Nachingwea, Liwale na Ruangwa na kusema kwamba msimu wa mvua umeshaanza katika maeneo mengi hapa nchi hivyo kwa kufanya usafi huo itasaidia kulinda miundombinu hiyo iliyotumia fedha nyingi za walipa kodi.
“Kila Meneja anapaswa kukagua na kufanya usafi kwenye madaraja na makalavati katika maeneo yake ili mvua zinaponyesha isikwamishe shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi endapo madaraja au makalavati yatasombwa na maji”.Alisisitiza
Alisema kutokufanya hivyo ni uzembe ambapo itaisababishia Serikali hasara kwa kutenga tena fedha za ujenzi na kwamba hatosita kuchukua hatua kali kwa Mameneja hao kwa uzembe utakaopelekea madaraja kusombwa na mafuriko, agizo ambalo alilitoa hivi karibuni wakati alipotembelea Wilaya za Nachingwea, Liwale na Ruangwa Mkoa wa Lindi.
Naye, Meneja wa TARURA Mkoa wa Lindi Mhandisi Fanuel Kalugendo aliahidi kusimamia na kufuatilia agizo la Mtendaji Mkuu na kutoa taarifa baada ya kazi kukamilika.
Mhandisi Seff yupo ziara ya kikazi ya kufuatilia miradi ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara mkoani Lindi.