Watu 56 wamefikishwa katika Mahakama ya mwanzo iliyopo Mkuyuni Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kucheza kamari, wizi, uvivu na uzembe unaosababisha kujiweka mbele ya hadhara katika hali inayopelekea uvunjifu wa amani kinyume na kifungu cha 176 (e).
Washtakiwa hao, wanadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 12, 2024 katika eneo la Buhongwa na Nyegezi Wilayani humo majira ya saa 5 usiku ambapo walikamatwa na askari Polisi waliokuwa doria maeneo.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya mwanzo Mkuyuni, Maryness Kilenzi na Hakimu Mkazi John Mugonya, Mwendesha mashtaka Koplo Dorothy Mauma alisema, Washtakiwa walitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 89(1) (b), 176(e), 258(1) na 265 katika kesi ya jinai namba 1727, 2024 , 1725, 2731,1713, na 1730 za mwaka 2024.
Kwa mujibu wa kifungu cha 176 (e) watuhumiwa wakikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo cha miezi mitatu gerezani, kulipa faini au vyote kwa pamoja ambapo hata hivyo washtakiwa wote wamekana mashtaka huku 43 kati yao wakipelekwa rumande kwa kushindwa kukidhi masharti ya dhamanana kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 18, 2024.