Heldina Mwingira, Dar24 Media – Dar es Salaam.
Dunia inatafsiri Ukatili wa kijinsia kwa namna mbalimbali, lakini sote tunatambua kwamba Ukatili ni hali ya kusababisha kwa makusudi mateso na kukosesha raha dhidi ya mtu mwingine, ilihali suluhisho la wazi linaweza kupatikana kwa urahisi.
Kwa mujibu wa kitabu kilichoandikwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake – TAMWA, kinaonesha kuwa Ukatili wa kijinsia ni kitendo chochote ambacho kinaweza kusababisha madhara ya kimwili, kingono, kisaikolojia au mateso kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kutishiwa maisha, kunyimwa uhuru, iwe hadharani au kwa kificho.
Kuna aina nyingi za Ukatili, kama vile wa kisaikolojia, wa kingono, wa kimwili na hata wa kiuchumi na kadiri matukio ya ukatili yanavyozidi kuongezeka, kuna haja ya mamlaka zinazohusika Ulimwenguni ikiwemo Tanzania kutakiwa kuchukua hatua za kuboresha mifumo ya kupokea na ufuatiliaji.
Ingawa Dunia inapoongelea kuhusu ukatili wa Kijinsia, mara nyingi hulenga upande wa wanawake lakini wahanga wanaweza kuwa jinsia zote ambao kiuhalisia hukutana na changamoto kubwa kama kupuuzwa au kukosa usaidizi wa kutosha, hali inayowakatisha tamaa na kuwafanya waone sauti zao hazisikilizwi na kuthaminiwa.
Ushughulikiaji wa matukio haya kwa uzito na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa, inaweza kuchangia kupungua kwa Matukio ya Ukatili mtandaoni na kuhakikisha Usalama wa Mtandaoni kwa Watuamiaji wote, ikikumbukwa kwamba harakati za kupinga ukatili zilipata nguvu zaidi mwaka 1995 katika mkutano wa Beijing ulioazimia mambo mbalimbali ikiwemo kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake.
Hawakuzungumzia kuhusu ukatili kwa jinsia ya kiume lakini leo hii tunashuhudia ripoti mbalimbali kwamba Wanaume pia hukumbwa na adha hiyo ya Ukatili wa Kijinsian ikidhihirishwa na ripoti ya haki za binadamu iliyoeleza juu ya ongezeko la vitendo vya ukatili kwa upande wa wanaume kufikia asilimia 10 mwaka 2023 kutoka asilimia 6 mwaka 2022.
Mwandishi wa Makala hii aliangazia ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanaume kwa kuzungumza na mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, Kelvin Joseph ambaye alisema mara nyingi hupigwa na wake zao, lakini kutokana na mtazamo wa jamii yetu wanashindwa kusema popote.
Anasema, “Jirani yangu alikuwa anapigwa na mke wake mara kwa mara muda wa usiku, ila kutokana na kuona aibu alikuwa anashindwa kusema anabaki anaumia rohoni mwisho wake akafariki ghafla kwa shinikizo la damu, hapo ndipo ikaja kugundulika baada ya majirani kuanza kutafuta chanzo cha uhalisia wa kifo hicho.”
Raia mwingine ambaye alitaka jina lake lihifadhiwe alisema amewahi kupitia ukatili kwa kubakwa na mwanamke ingawa hakutaka kufafanua ni jinsi gani tukio hilo lilimkuta akisema, “iliniwia vigumu kusema kwasababu kwanza ni aibu pia hamna mtu ambaye angeniamini na tukumbuke tunaishi kwenye jamii yenye utamaduni ambao mwanaume anaonekana ni mwenye nguvu hatakiwi kulia wala kulalamika ikanipasa kunyamaza na kukabiliana na jambo hili mimi mwenyewe.”
Uhalisia ni kwamba Wanaume hupata ukatili wa kijinsia kwa viwango vya juu kuliko watu wanavyotambua au kuzungumzia na mara nyingi mashambulizi haya hutokea kabla ya umri wa miaka 18 kwa Mvulana au Mwanamume na mara nyingi wahanga huwajua fika washambuliaji husika.
Wanaume wanaweza kubakwa wakiwa watu wazima na kunyanyaswa kingono wakiwa watoto, hupata dalili sawa na Wanawake baada ya kudhulumiwa kingono, hivyo ni muhimu kwa Mwanamume kupokea ushauri nasaha kwa kiwewe cha kijinsia kama ilivyo kwa mwanamke kwani unyanyasaji wa kijinsia una madhara na kunyanyaswa ukiwa mtoto haimaanishi kuwa utakua mhalifu.
Lakini zipo sababu ambazo huwafanya Wanaume wasitafute ushauri au msaada mara nyingi kama kama ilivyo kwa Wanawake, haswa kwa maswala ya unyanyasaji wa kijinsia, kutokana na imani kwamba Wanaume wanataka ngono kila wakati na hawatakataa kukutana na ngono.
Aidha, makubaliano na dhana za kijamii kwamba uzoefu wa ngono wa mapema ni sehemu ya kawaida ya maisha ya Mvulana na Wanaume unaweza kuhoji mwelekeo wao wa kijinsia ikiwa walinyanyaswa kingono hivyo huweza kuchanganyikiwa na kupata hasira juu ya kupoteza udhibiti wa miili yao na majibu yoyote ya kimwili waliyokuwa nayo kwa kushambuliwa.
Uzoefu unaonesha kuwa kesi za namna hii hutokea mara moja moja na sio kwasababu hamna anayefanyiwa ukatili, bali ni kukosekana kwa uthubutu ingawa wapo waliowahi kusema mfano wa kesi moja ya Mwanaume (jina linahifadhiwa), aliwahi kulalamika kunyimwa unyumba miezi nane mfululizo kiasi aliamua kufika kwa Afisa mmoja wa Ustawi wa Jamii kuomba talaka.
Japo alithubutu kusema lakini bado alikuwa anakumbwa na aibu kutokana na Afisa Ustawi yule kuwa ni jinsia ya kike na alisema alikuwa akiona ni jambo lisilozoeleka, ila alipata usaidizi mpaka familia yake ikaendelea vyema, jamboa ambalo ni mfano wa kuigwa kwa Wanaume wengine wanaofanyiwa ukatili.
Gerald David yeye ni Mwanasaikolojia, alipoulizwa kuhusu jambo hili alisema Wanaume wengi wanafanyiwa ukatili kama vile kupigwa, kubakwa, kunyimwa unyumba na hata ukatili wa kingono kwamba ili wapate fursa fulani hasa Madereva na Wafanyakazi wa ndani, hupelekea wengi wao kupata msongo wa mawazo na kusababisha kujiua au kufa ghafla kwa shinikizo.
Anatoa rai kwa Wanaume kuzungumza yaliyo moyoni mwao ili kupata matibabu na haki zao za kisheria akisema ni muhimu jamii ibadilishe mtazamo juu ya suala ya ukatili wa kijinsia kuwa ni Wanawake pekee walio wahanga.
Hata hivyo, kutokana matukio ya namna hii, imemlazimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima kuwataka wanaume kutoa taarifa kwenye mamlaka husika kuhusu ukatili wanaofanyiwa, ili kutokomeza matukio ya namna hiyo.
Alisema ukatili haufanywi kwa Wanawake na Watoto tu lakini hata kwa makundi mengine ikiwemo Wanaume lakini wengi wao wamekuwa wakikaa kimya akisema Wizara itaendelea kuchukua jitihada zote kuhakikisha ukatili unatokomezwa kwa makundi yote, lakini jamii pia ina jukumu la kuwalinda makundi yote.
“Wanaume msione aibu, muache kukaa kimya dhidi ya vitendo vya ukatili mnavyofanyiwa. Toeni taarifa mapema kwa mamlaka husika muweze kupata msaada ili kuzuia madhara zaidi kutokea,” alisema Gwajima.
Katika kuangazia utatuzi wa changamoto ya Wanaume kiukatili, Shirika la Save the Community Organisation – SCO, limesema Mwanaume akifanyiwa ukatili wa kijinsia anaweza akaripoti katika Serikali ya Kijiji au mtaa anaoishi, kwa Viongozi wa Dini unapoabudu, kwenye vituo vya msaada wa Sheria, Ofisi ya Ustawi wa Jamii au Polisi kwenye dawati la jinsia.
Wanasema, inashauriwa kuripoti mara unapofanyiwa kitendo cha Ukatili, huku muhusika akiwa na ushahidi wa tukio husika na kusisitiza kuwa ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanaume uwe wazi kwani ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha harakati zinazofanywa kwa Wanawake pia zifanyike kwa Wanaume.
Hata hivyo, kwa takwimu za Umoja wa Mataifa hili bado haliondio ukweli wa matokeo ya ripoti nyingi za unyanyasaji wa nyumbani zinatolewa na Wanawake, ikionekana kuwa theluthi ya Wanawake wote na Wasichana hupitia unyanyasaji wa kimwili na kingono wakati mmoja katika maisha yao.
Ni wazi sasa jamii kwa pamoja inatakiwa kushikamana na kupaza sauti, ili wenye mamlaka waweze kukomesha ukatiliwa aina hii bila kujali jinsia.