Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ameshangazwa na idadi ndogo ya waombaji wa nafasi za kazi  kada ya Afya katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Lindi na Mtwara, huku Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma ikiwa na idadi kubwa ya waombaji ikilinganishwa na uhitaji.

Sangu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na  Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mkoani Katavi, ikiwa ni muendelezo wa  kliniki ya kimkakati ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili  Watumishi hao.

Amesema, licha ya tatizo kubwa la ajira linalowakumba vijana wengi  lakini bado waombaji hao  wanataka kuanza  kufanya  kazi katika Majiji makubwa jambo ambalo ni gumu huku akitolea mfano Mkoa wa Kigoma ambao mahitaji yake halisi ya waliotakiwa kuajiriwa katika kada ya afya ilikuwa ni 400, lakini waombaji walikuwa hawazidi 200 huku Mikoa ya Lindi, Mtwara na Katavi nako idadi ni ndogo ukilinganisha na uhitaji.

Kufuatia hatua hiyo, Sangu ametoa wito kwa wazazi kuwashawishi watoto wao kuomba ajira pindi zinapotangazwa  katika mikoa hiyo kwani uwezekano wa kupata ni mkubwa ukilinganisha na mikoa kama vile Arusha na Dodoma ambako ushindani ni mkubwa na kuwaonya watakapangiwa kuwa Serikali haitawavumilia watakapoanza kuomba uhamisho kabla ya kufanya kazi kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.

Amesema, mikoa hiyo haina tofauti na Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na Arusha kwani ina fursa za kiuchumi pamoja na miundombinu iliyoboreshwa, huku  akiwataka wenye uhitaji wa ajira kuchangamkia ajira zinapotangazwa kwenye mikoa hiyo.

Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Abert Msovela alisema licha ya uwepo wa fursa za kiuchumi katika mkoa huo lakini bado idadi ya Watumishi wa Umma wanaotuma maombi ya kutaka kuhama ni mengi na kuwaasa Watumishi kubadili kasumba hiyo kwani Mkoa wa Katavi kwa sasa ni Mkoa wa kutimiza ndoto za kila Mtumishi mwenye kutaka kujikwamua kiuchumi kutokana na uwepo wa fursa lukuki za kiuchumi ikiwemo ardhi yenye rutuba.

Hatua hiyo, inakuja kufuatia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuweka utaratibu wa kuomba ajira katika mkoa husika kulingana na uhitaji ambapo Mwezi Juni 2024, ilitangaza jumla ya nafasi za kazi 9483 za kada ya afya ambapo kila muombaji alilazimika kuomba ajira katika mkoa ambao atafanya kazi endapo atafanikiwa kupita kwenye usaili.

Balozi Kombo aongoza Mkutano wa dharura Kamati ya Mawaziri SADC
Polisi: Mnaolala Nyumba za Wageni andikeni taarifa sahihi